SHIME: KAMBI YA TUNISIA IMEWANOA VEMA SERENGETI GIRLS




MONASTIR, Tunisia

Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, ‘Serengeti Girls’, Bakari Shime, ameeleza kuridhishwa na kambi ya siku 10 mjini Monastir, akisema imeimarisha kikosi chake kuelekea mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia. 

Katika kambi hiyo nchini Tunisia, Serengeti Girls imecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji wao, ambapo walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza na kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa pili.

Shime alibainisha kuwa matokeo hayo ni chanya kwa timu yake kwani yamewapa benchi la ufundi nafasi ya kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa mechi za kimashindano. 

Alisisitiza kuwa mechi hizo dhidi ya Tunisia zilikuwa darasa tosha, hasa kwa kuzingatia kuwa idadi kubwa ya wachezaji kikosini hapo ni wageni na ndiyo mara yao ya kwanza kuitwa kwenye timu ya taifa na kuonja ladha ya soka la kimataifa.

Kikosi hicho cha Serengeti Girls kilitarajiwa kuondoka nchini Tunisia jana kuelekea Botswana kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa hatua ya kufuzu utakaopigwa Aprili 10 katika mji wa Francis Town.

Kocha Shime ameelezea kuwa na imani kubwa na vijana wake, akiamini kuwa utulivu na uzoefu walioupata kaskazini mwa Afrika utawasaidia kupata matokeo mazuri ugenini kabla ya kurudiana nchini Tanzania baadaye mwezi huu.

Mshindi wa jumla katika mchuano huo kati ya Tanzania na Botswana atapambana na Afrika Kusini, ambayo imesonga mbele kufuatia mpinzani wao, Jamhuri ya Afrika ya Kati, kujitoa katika mashindano hayo. Serengeti Girls wanatafuta nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika nchini Morocco, ikiwa ni mara yao ya pili baada ya kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufuzu mashindano hayo mwaka 2022 nchini India.

No comments