Kanye West ayakanyaga Uingereza, Waziri Mkuu apinga uwepo wake
LONDON, Uingereza
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ameonyesha wasiwasi wake mkubwa kufuatia mpango wa rapa kutoka nchini Marekani, Kanye West, kutumbuiza jijini London mwezi Julai mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja kutokana na historia ya msanii huyo ya kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Wayahudi na kusifu itikadi za Kinazi.
Starmer aliliambia gazeti la The Sun siku ya Jumamosi kuwa, inasikitisha kuona Kanye West—ambaye sasa anajulikana kama Ye—amepewa nafasi ya kutumbuiza katika tamasha la Wireless, licha ya vitendo vyake vya huko nyuma. Alisisitiza kuwa chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism) ni jambo la kuchukiza na lazima likabiliwe kwa nguvu zote.
Pepsi Yajiondoa, Shinikizo Laongezeka
Kufuatia utata huo, kampuni ya vinywaji ya Pepsi, ambayo ilikuwa mdhamini mkuu wa tamasha hilo, imetangaza kujiondoa rasmi. Ingawa Pepsi haikutoa sababu ya moja kwa moja ya uamuzi huo, hatua hiyo imekuja huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wanaharakati.
Taasisi ya hisani ya Campaign Against Antisemitism imemtaka Waziri Mkuu Starmer kuzuia kuingia kwa Kanye West nchini humo. Taasisi hiyo imesema kuwa Uwepo wa msanii huyo si kwa manufaa ya umma, ikizingatiwa kuwa hata nchini Ufaransa, Meya wa Marseille alishatangaza kuwa Kanye hakaribishwi kwa tamasha lililopangwa kufanyika Juni.
Historia ya Utata
Kanye West, mwenye umri wa miaka 48, amekuwa akikosolewa vikali tangu mwaka jana baada ya kuachia wimbo uliolenga kusifu utawala wa kidikteta wa Adolf Hitler, kitendo kilichopelekea wimbo huo kupigwa marufuku katika majukwaa makubwa ya muziki duniani.
Hata hivyo, Kanye amewahi kuelezea masikitiko yake juu ya matamshi hayo, akidai kuwa yalitokana na changamoto za afya ya akili (bipolar disorder) zinazomkabili. Mpaka sasa, waandaaji wa tamasha hilo, kampuni ya Live Nation, hawajatoa tamko lolote kuhusiana na malalamiko hayo yanayoendelea kufukuta.

Post a Comment