Wenye Jeuri na Mpira Watinga Robo Fainali Kombe la CRDB
Vita ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB imepamba moto baada ya miamba Simba SC, Singida Black Stars, na TRA United, kufanikiwa kukata tiketi na kutinga hatua ya robo fainali.
Timu hizi zimeungana na vigogo wengine baada ya kuonesha viwango vya hali ya juu vya soka na kupata matokeo chanya katika michezo yao ya hatua ya 16 bora iliyopigwa katika viwanja tofauti nchini.
Simba Yapindua Meza Arusha
Katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Simba walilazimika kufanya kazi ya ziada baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema dakika ya tisa lililofungwa na Khleffin Hamdoun wa Dodoma Jiji.
Simba walirudi kipindi cha pili kwa kasi na kupindua meza kupitia mabao mawili ya Seleman Mwalim (dakika za 54 na 67) pamoja na bao la Anicet Oura (dakika ya 60), na hivyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Kichapo cha Mbwa Mwizi Singida
Nao Singida Black Stars walitumia vyema uwanja wao wa nyumbani wa Airtel mkoani Singida kwa kutoa kipigo kizito cha mabao 5-1 dhidi ya Mbeya City.
Mashambulizi ya Singida yalikuwa mwiba, yakiongozwa na Khalid Aucho aliyefungua karamu ya mabao, akifuatiwa na Lamine Jarjou, Ibrahim Imoro aliyepiga "double" (mabao mawili), na Horso Mwaku.
Mbeya City walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Daniel William dakika ya 81.
TRA United Yaitupa Nje Namungo
Mshangao mwingine umetokea kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, ambapo TRA United walifanikiwa kuwatoa wenyeji wao Namungo FC kwa mabao 2-0.
Mabao ya washindi yalipatikana mapema kupitia kwa Ally Ng’anzi dakika ya 12, huku Denis Nkane akipigilia msumari wa mwisho dakika ya 58, matokeo ambayo yamewahakikishia nafasi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo mikubwa.
Ramani ya Robo Fainali Inavyoonekana
Hadi sasa, timu saba tayari zimeshafuzu hatua hiyo ya robo fainali ambazo ni:Simba SC,Singida Black Stars,TRA United, JKT Tanzania,Mashujaa FC,Coastal Union na Yanga SC (Bingwa Mtetezi).
Nafasi ya nane na ya mwisho itajulikana baada ya mtanange mkali kati ya Azam FC dhidi ya Fountain Gate.
Bingwa wa michuano hii atapata heshima ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup)

Post a Comment