JWTZ:OLE WAO WATAKAOJARIBU KUVURUGA AMANI



JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa msimamo mkali kuhusu hali ya amani nchini na kuwataka wananchi kupuuza wito wowote unaohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani, likisisitiza kuwa litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda nchi, katiba na mamlaka ya dola kwa mujibu wa sheria.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Sylvester Mangure kutoka makao makuu ya jeshi aliyesema hali ya usalama nchini na katika mipaka ya Tanzania inaendelea kuwa shwari, jambo lililowezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku za kujenga uchumi na maendeleo ya taifa.

Mangure aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na utulivu, huku akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia kuendelea kuwepo kwa mazingira salama nchini.

Hata hivyo, alisema kuna watu wasioitakia mema nchi wanaoendelea kuhamasisha na kupotosha wananchi kushiriki katika vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, huku wakilihusisha JWTZ kwa madai yasiyo ya kweli kwamba litawalinda watakaoshiriki katika vitendo hivyo.

Alisema vurugu na ghasia zinazohamasishwa zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa washiriki na wananchi wengine wasiokuwa na hatia, ikiwemo kupoteza maisha, kujeruhiwa, kuharibika kwa mali, kuvurugika kwa shughuli za uzalishaji na kuathiri uchumi wa Taifa.

Kutokana na hali hiyo, JWTZ limewataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu na kupuuza wito wowote unaochochea vurugu, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayeshiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani.

Mangure alifafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, JWTZ ina wajibu wa kulinda usalama wa nchi na wananchi na pia lina mamlaka ya kusaidia mamlaka za kiraia wakati wa vurugu, ghasia au matukio mengine ya uvunjifu wa amani pale litakapohitajika kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa na mamlaka husika endapo watabaini viashiria vya uchochezi au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Mangure aliwahakikishia wananchi kuwa JWTZ itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, utii, uaminifu na uhodari, kwa kuzingatia viapo walivyoapa, huku likiendelea kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kulinda amani, utulivu, umoja na maendeleo ya taifa.

No comments