SIRI YA AMANI YA MOYO: NJIA YA MARIDHIANO NA MSHIKAMANO KWA VIJANA WA LEO




Katika kipindi hiki ambacho Taifa linapambana kusaka mshikamano na maridhiano ya dhati, wataalamu wa saikolojia na stadi za maisha wameibuka na darasa zito linalolenga kuwasaidia vijana kupata amani ya ndani kama msingi wa umoja wa kitaifa. 

Mshauri Mwelekezi wa Stadi za Maisha, Gloria Lema, amebainisha kuwa safari ya kuelekea kwenye furaha ya kweli inaanza na hatua moja muhimu ya kila kijana 'kujitambua' ili kufahamu mambo yanayompa ridhiko la kudumu. 

Lema anaeleza kuwa kijana anapojitambua na kutengeneza mtindo wa maisha unaoendana na mahitaji yake halisi, anajiepusha na msongo wa mawazo unaotokana na ushindani usio na tija, jambo ambalo ni nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye kuelewana na kuvumiliana.

Ufafanuzi huo unaenda mbali zaidi kwa kuangazia kuwa amani ya moyo ni zao la hali ya ndani ya mwanadamu na si milki ya vitu vya anasa kama ambavyo wengi wanadhani sasa. 

Mtaalamu wa Saikolojia, Cosmas Madulu, amesisitiza kuwa kijana ana uwezo wa kujitengenezea furaha ya kudumu bila kujali kiasi cha mali alichonacho, kwani furaha ya kweli ni matokeo ya nafsi, roho, na mwili kukamilishana kwa ushirikiano.

Madulu anasema kuwa kijana mwenye utulivu wa ndani anakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika mchakato wa maridhiano na mshikamano wa kijamii kwa sababu moyo wake haujajawa na chuki wala kinyongo kinachosababishwa na shinikizo la maisha.

Hata hivyo, mjadala huo umeibua hisia mseto miongoni mwa wananchi ambapo baadhi yao wanaamini kuwa siri ya amani hiyo imejificha kwenye misingi ya kiimani. 

Wakati wataalamu wakijikita katika sayansi ya akili, sauti za wadau wengi zimesikika zikielekeza kuwa majibu ya kudumu ya amani ya moyo yanapatikana katika vitabu vitakatifu vya Biblia na Quran, na kwamba maelezo mengine ni simulizi tu. 

Muingiliano huu wa mawazo kati ya saikolojia na imani ni kielelezo tosha kuwa vijana wa leo wanahitaji dira inayowaunganisha ili waweze kuwa na amani ya moyo itakayolisaidia Taifa kusimama kwa pamoja katika upendo, mshikamano, na maridhiano ya kweli.

No comments