MY SON' YAWEKA REKODI YA KIBABE: YAZINDUWA KWA KISHINDO MLIMANI CITY




Zulia jekundu liligeuka kuwa uwanja wa ushindi mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Century Cinemax, Mlimani City, wakati filamu ya Kitanzania ya ‘My Son’ ilipozinduliwa rasmi kwa kishindo cha aina yake. 

Uzinduzi huo uliokusanya vigogo wa serikali, mastaa wa filamu na wadau wa sanaa, umekuja huku kazi hiyo ikiwa tayari imetikisa anga la Tuzo za Filamu Tanzania (TAFFA) msimu wa 2025/2026 kwa kunyakua jumla ya tuzo sita, ikiwemo taji la Filamu Bora ya Mwaka na Muongozaji Bora wa Kiume.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Gervas Kasiga, aliipongeza kampuni ya Jitu la Msitu Entertainments chini ya Mkurugenzi Isarito Mwakalindile, kwa kuleta mapinduzi ya ubora yanayoweza kushindana katika soko la kimataifa. 

Dk. Kasiga alibainisha kuwa nidhamu ya hali ya juu na ubunifu uliotukuka wa muongozaji Ramar King, ndiyo siri iliyofanya ‘My Son’ kupata nafasi ya kipekee katika kumbi za kisasa za sinema, huku akiahidi kuwa serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa Jumba Changamani la Filamu ili kukuza tija kwa wasanii.

Kazi hiyo ambayo imesifiwa kwa kuwa na picha zenye rangi zilizopangiliwa, sauti ya kiwango cha juu, na mandhari zinazovutia, imevunja rekodi nyingine baada ya kuingia rasmi katika mauzo ya jukwaa la kidijitali la Azam Max kwa mwaka 2026. Hatua hii ni ushindi mkubwa kwa sinema ya nyumbani, kwani itaiwezesha ‘My Son’ kupasua anga na kuwafikia wapenzi wa filamu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kupitia mifumo ya kisasa ya kitehama, hivyo kuongeza thamani ya kibiashara kwa kazi hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya filamu waliohudhuria uzinduzi huo wameitaja ‘My Son’ kama kielelezo kipya na cha kisasa cha filamu za mapigano (action) nchini, wakisifu ufundi wa hali ya juu katika mpangilio wa mapigano na mnyororo wa simulizi unaomfanya mtazamaji kubaki kwenye kiti mpaka mwisho. Mafanikio haya yanatajwa kuwa chachu kwa watayarishaji wengine nchini kuachana na mazoea na kuanza kuwekeza katika vifaa vya kisasa pamoja na maarifa ya kitaalamu.

Katika kuhitimisha sherehe hizo za uzinduzi, Bodi ya Filamu ilisisitiza wajibu wake kama mlezi kwa kuahidi kuendelea kutoa mafunzo ya fani na biashara ya filamu. Lengo ni kuhakikisha kuwa wasanii wa Tanzania hawazalishi tu maudhui ya kuburudisha, bali wanatengeneza bidhaa zenye thamani kubwa inayoweza kuingia kwenye masoko makubwa ya dunia na kuitangaza Tanzania kama kitovu kipya cha sinema barani Afrika.


No comments