Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, January 15, 2024

Kikosi cha Serengeti Girls hadharani


 Kikosi cha timu ya Taifa Wanawake U17 kitakachoingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Zambia kufuzu Kombe la Dunia

Sunday, September 17, 2023

Changarawe atwaa medali ya fedha

Changalawe na Rais wa TBF


Na Rahel Pallangyo

BONDIA wa Tanzania, Yusuf Changarawe amepata medali ya fedha baada ya kushindwa pambano lake la fainali la mashindano ya kusaka nafasi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa 2024.

Changarawe alipigwa na bondia kutoka Misri, Abdelrahman Abdelgawwad katika pambano la uzito wa kilo 80 na hivyo kukosa nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika Michezo ya Olimpiki.

Bondia huyo na wengine wa Tanzania sasa watasubiri mashindano mengine mawili yatakayofanyika Italia na Thailand Februari na Aprili mwakani ili kusaka tena nafasi ya kwenda Paris katika Olimpiki.

Tanzania katika mashindano hayo ya kufuzu huko Dakar, Senegal ilipeleka mabondia sita, wanne wa kiume na wawili wa kike, ambao walikwenda kusaka nafasi ya kwenda Paris.

Mbali na Changarawe, mabondia wengine wa Tanzania ni Musa Malegesi (kilo 92), Mwalami Salum (kilo 57) na Abdallah Mohamed (kilo 51) wakati wanawake ni Zulfa Macho (kilo 50) na Grace Mwakamele (kilo 60).

Mkuu wa msafara wa timu hiyo alikuwa Rais wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT), Lukelo Wilillo. Viongozi wengine ni Mashaga (kocha msaidizi), Samuel Kapunga (Kocha Mkuu) na Aisha George (matroni).

Wednesday, September 13, 2023

NBC CHAMPIONSHIP LEAGUE YALAMBA UDHAMINI MNONO
Na Rahel Pallangyo 

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)  limeingia mkataba wa miaka mitatu na  TV 3 wenye thamani ya Sh. Milioni 613, kwa ajili ya haki za kurusha NBC Championship League.

Udhamini wa TV 3 umekuja siku chache baada ya kupata mdhamini mkuu ambaye ni benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni miaka 11 imepita bila mdhamini.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, Rais wa TFF Wallace  Karia alisema wameingia mkataba wa kuonesha mubashara NBC Championship League kwa sababu inawasaidia kila kitu kuwa hadharani na kupunguza malalamiko yasiyo na msingi.

Alisema watafanikiwa kuona timu ambazo zinatumia mambo maovu kwa ajili ya kujinufaisha lakini pia kubaini malalamiko ya timu zinazolalamika kufanyiwa maovu na kuwataka viongozi wa klabu kutumia fursa hiyo kujitafutia wadhamini binafsi.
“Nina imani wadhamini wetu hao hawatajutia kabisa kufanya kazi na TFF na nitahakikisha wanapata kipaumbele inapotokea fursa nyingine," 
Karia alisema ligi hiyo ni kati ya ligi ngumu nchini na kuishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani.

"Kuonesha kwa Ligi Kuu kupitia Azam TV imekuwa hamasa kubwa kwa kuifanya iwe bora, matarajio yangu kwa mkataba huu tulioingia na TV 3 kwa ajili ya kuonesha mechi ya Championship itafanya pia kuwa bora zaidi na kuleta wadhamini wengine,” alisema Karia.
“Tutakuwa wakali kwa klabu ambazo   hazijajianda kucheza daraja la juu, niwaombe wapambane kutafuta wadhamini ili kujimudu katika ligi wanayoshiriki, TFF sio kazi yao kuwatafutia klabu wadhamini,” alisema.
Naye Msimamizi wa vipindi wa TV3, Emmanuel Sikawa alisema mkataba huo ni hatua kubwa kwao kwa sababu wanatarajia kuonesha mechi 170 kati ya 240 ambazo zitachezwa katika ligi hiyo.
Alisema ligi hiyo itaonueshea katika chanel mbili ambazo ya 197 kwa upande wa Dish na 131 kwa Antena, ambazo zinaruka nchi saba.
“Tunatarajia ligi  itaoneshwa katika mataifa hayo saba ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda , Afrika Kusini, Uganda, Burundi na Msumbiji ikiwa ni lengo la kutangaza ligi hii na wachezaji kuonesha vipaji vyao na kuonekana kujiuza kwa kutazamwa,” alisema Sikawa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).

Tuesday, September 12, 2023

DK NDUMBARO AMPA KARIA MAUA YAKE WAKISAINI MKATABA NA SANDALAND FASHION WEAR LTD

 
Na Rahel Pallangyo

SERIKALI imepongeza uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuingia mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya Sandaland Fashion Wear LTD wenye thamani ya Sh bilioni 3 kwa ajili ya kuzivalisha timu zote za Taifa.

Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, Dar es Salaam juzi baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo.

“Nashukuru sana uongozi wa TFF chini ya uongozi wa ndugu yangu Wallace Karia, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, TFF inaingia mkataba na mtengenezaji jezi kwa ajili ya timu zote za Taifa, tunaweza kulichukulia jambo hilo kama dogo sana lakini halijawahi kufanyika na linafanywa na TFF chini ya jemedari Wallace Karia,”

“Nasisitiza haya kwa sababu sisi Watanzania ni wazuri sana wa kukosoa lakini tunakuwa wachoyo kusifia pale jambo zuri linapofanyika na kwa mara ili timu zote za taifa ziwezi kupata jezi rasmi zinazotengenezwa na kampuni yenye heshima kubwa hapa Tanzania,” alisema Dk Ndumabaro.

Naye Rais wa TFF Wallace Karia alisema mkataba huo utahusisha timu zote za Taifa na katika mkataba huo watakuwa wanapewa jezi bure kwa timu zote na watakuwa wanapata fedha.

“Leo tunatimiza ahadi yetu ya kuongeza wadhamini zaidi. Mkataba huu ni wa kihistoria kwani tutakuwa tunapata jezi bure na pia tunapata fedha jambo halijawahi kutokea,” alisema Karia.

Pia Karia alisema huo ni utekekezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka wawekezaji wazawa kupewa nafasi zaidi ambapo alisema atakuwa anawalegezea kwenye kodi.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Sandaland Fashion Wear LTD, Yusuph Yenga alisema kampuni hiyo ina uzoefu wa kutengeneza jezi na kuahidi kuwa jezi hizo zitakuwa na ubora na viwango vya hali ya juu.

Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio alipongeza TFF kwa mafanikio waliyopata katika kipindi cha uongozi wa Karia.

“Sisi Tume ya ushindani ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafanikiwa kwa kuweka mazingira mazuri na nimefurahi kuona kampuni ya wazawa imeshinda zanuni ya kutengeza jezi za timu za Taifa,”

BONDIA WATATU WAFUZU ROBO FAINALI, DAKAR SENEGAL

Bondia Abdallah Abdallah 'Katoto'


Bondia machachari Abdallah Abdallah 'KATOTO'  amefanikiwa kushinda kwa kishindo dhidi ya mpinzani wake Abdallah Saied Nasser EMAM kutoka Misri kwa points za majaji wote watano (5-0) katika uzani wa 51kg ya bout no. 114.

Sasa jumla ya Watanzania watatu wametinga hatua za robo fainali akiwepo Yusuf Changalawe, Grace Mwakamele na Katoto.

Bondia mwingine wa Tanzania aliyecheza jana awali Musa Maregesi alipoteza kwa pointi dhidi ya mwenyeji kutoka Senegal Kebe Karamba katika uzani wa 92kg ya bout.l no 99.

Leo ni  mapumziko katika michezo hii ya kuwania nafasi za kufuzu kushiriki Olimpiki ya Paris 2024 inayoendelea Dakar, Senegal.

BARNABAS ELIAS BALOZI WA HAKIMILIKIWaziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro akimkabidhi Cheti cha Utambulisho Msanii Barnaba  Elias ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Hakimiliki Tanzania kwenye hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya COSOTA na Bodi ya Bodi Filamu Septemba 12, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limehudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamis Mwinjuma, Katibu Mkuu, Saidi Yakubu na Viongozi wa Taasisi hizo na Mashirikisho ya Sanaa.


DK NDUMBARO AZINDUA BODI MBILI, AZIPA JUKUMU LA KUONGEZA MAPATO

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro akizungumza kwenye hafla ya kuzindua bodi za COSOSTA na Bodi ya Filamu

Naibu Waziri Hamis Mwinjuma

Katibu Mkuu Said Yakubu

Waziri Dk Ndumbaro, Naibu Hamisi Mwinjuma, Katibu Mkuu, Said Yakub na wajumbe wa bodi za COSOSTA na Bodi ya Filamu


Na Rahel Pallangyo

Wajumbe ya Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOSTA) na Bodi ya Filamu Tanzania wametakiwa kuhakikisha sekta ya sanaa inatoa ajira za kutosha na wananchi wanafaidi matunda ya kazi zao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro wakati akizindua bodi za taasisi hizo  Dar es Salaam leo 

“Wizara hii ina dhamana kubwa na watekelezaji wa kazi zake ni taasisi zinazosimamiwa na Bodi, kazi yenu ni kuhakikisha taasisi mnazozisimamia zinakua kiuchumi ili kukuza Pato la Taifa na uchumi wa wadau wa sekta yetu ya Sanaa ambayo imekua kwa asilimia 19 ”amesisitiza Waziri Dkt. Ndumbaro.

Awali akimkaribisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro kuzindua Bodi hizo, Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma amewahimiza wajumbe wa bodi hizo kutekeleza wajibu wao ili kuleta uhalisia na utofauti wa utendaji wa kazi wa taasisi hizo kabla ya uteuzi na baada ya kuingia madarakani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesisitiza kuwa sekta ya Sanaa nchini imekuwa na Tanzania ni ya pili Afrika ambapo inazalisha filamu 2000 kwa mwaka sawa na wastani filamu sita kwa siku.

Ameongeza kuwa Sekta hiyo imefanikiwa kuzalisha wingi wa filamu na kuwahimiza wajumbe hao kushirikiana na taasisi wanazoziongoza ili kujikita kuzalisha kazi bora ambazo zitakuwa chanzo adhimu cha mapato kwa wasanii na taifa kwa ujumla.

Aidha, Yakubu amezitaka Bodi hizo kuhakikisha Taasisi zinaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka nje ya nchi kupitia kazi za Sanaa ambazo zinazooneshwa katika nje ya mipaka ya Tanzania na kuongeza ushirikiano na Taasisi zenye majukumu yanayofanana nayo.

Wakizungumza kuhusu uzinduzi wa Bodi hizo,  Mwenyekiti wa Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOSTA)  Victor Tesha na Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Dk. Mona Mwakalinga wamesema watahakikisha linakuwepo jukwaa ndani la kuonesha na kusambaza kazi za Sanaa ndani na nje ya nchi kama ilivyo majukwaa mengine na kusisitiza watasimia kuongeza  ubora katika filamu za Tanzania ili zipate soko kubwa zaidi duniani.