JAB yahimizwa kuanza kutekeleza mpango wa mafunzo
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imehimizwa kuanza kutekeleza mpango wa mafunzo ya kitaaluma kwa waandishi wa habari bila kusubiri kuwa na idadi kubwa ya washiriki.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, CPA Nyakaho Mturi Mahemba wakati alipotembelea banda la JAB katika Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba.
CPA Mturi alisema kwa sasa jambo la msingi ni kuanza utekelezaji ili kuendelea kujenga uwezo wa waandishi wa habari na kuimarisha taaluma ya habari nchini.
Katika ziara hiyo, CPA Nyakaho aliipongeza JAB kwa mafanikio makubwa ya kusajili waandishi wa habari 4,519 na kuwapatia ithibati waandishi 3,655 hadi kufikia tarehe 7 Julai, 2026.
Pongezi hizo zilitolewa baada ya kiongozi huyo kupata maelezo ya kina kutoka kwa Afisa wa Bodi hiyo, Bi. Editha Mayemba, kuhusu majukumu ya JAB ya kusimamia ithibati, kuimarisha maadili na weledi wa taaluma ya habari, pamoja na mipango ya sasa ya kuanza kutoa mafunzo kwa wanahabari.
Banda hilo la JAB lilitembelewa pia na wageni wengine mashuhuri wakiwemo Mtakwimu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Chacha Nyamuhanga, pamoja na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Abbas Kayanda.
Katika maelezo yake, Bw. Kayanda alisisitiza kwa nguvu zote umuhimu wa maafisa habari wa wizara na taasisi mbalimbali za umma kuhakikisha wanajisajili na kupata ithibati hiyo mapema iwezekanavyo, kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari nchini.



Post a Comment