DK HOMERA: SHERIA NI MSINGI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera, amesema Serikali inaendelea kuboresha sheria mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kuimarisha mazingira ya kiuchumi na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa urahisi na kwa wakati.Akizungumza katika Banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Dk Homera amesema maboresho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya Taifa.
Amesema lengo la maboresho hayo ni kuondoa vikwazo vinavyoathiri shughuli za kiuchumi, kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuimarisha utawala wa sheria, hatua zitakazochochea uwekezaji, biashara na maendeleo jumuishi.
Dk Homera amesema Wizara imeweka jopo la wataalamu wa sheria katika banda lake la maonesho kwa ajili ya kutoa huduma za ushauri wa kisheria, kusikiliza migogoro mbalimbali na kuwaelekeza wananchi kuhusu namna bora ya kutatua changamoto zao kwa mujibu wa sheria.
Ameongeza kuwa wananchi wanaohitaji kufungua mashauri katika vyombo vya utoaji haki wanapatiwa ushauri wa kitaalamu na, pale inapohitajika, huunganishwa na mawakili ili kuhakikisha wanapata huduma za haki kwa ufanisi na bila vikwazo visivyo vya lazima.
Aidha, Dk Homera amewahimiza wananchi kutembelea Banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maonesho ya 50 ya DITF ili kupata huduma za msaada wa kisheria bila malipo, ikiwemo ushauri kuhusu migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na masuala mengine ya kisheria.

Post a Comment