Papa Leo XIV Amchana Trump: "Wekeni Silaha Chini"
VATICAN CITY, Roma
Katika hotuba yake ya kwanza ya Pasaka tangu ashike hatamu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, ametumia fursa hiyo kutuma ujumbe mzito kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, akihimiza kusitishwa kwa mapigano na kusema, "Wale wenye silaha waziweke chini."
Papa huyo, ambaye ni mzaliwa wa kwanza wa Marekani kushika nafasi hiyo, alihutubia maelfu ya waumini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro.
Alionekana kukemea vikali vita vya Iran vinavyoongozwa na utawala wa Trump, akieleza kusikitishwa kwake na jinsi ulimwengu unavyoanza "kuzoea vurugu na kutojali mauaji ya maelfu ya watu."
Akizungumza, Papa Leo XIV mwenye umri wa miaka 70, alitoa wito kwa viongozi wenye mamlaka ya kuanzisha vita kuchagua njia ya amani. "Wale wenye uwezo wa kuanzisha vita na wachague amani! Siyo amani ya kulazimishwa kwa nguvu, bali amani inayopatikana kupitia mazungumzo," alisema kiongozi huyo katika baraka yake ya Urbi et Orbi (kwa mji na kwa ulimwengu).
Hotuba hiyo, ambayo ilikuwa fupi isivyo kawaida (dakika 15 badala ya dakika 30 za kawaida), ilijikita katika kumwelezea Yesu Kristo kama mfano wa "kutotumia nguvu kabisa." Papa alisisitiza kuwa amani ya kweli siyo tu ukimya wa silaha, bali ni kuachana na tamaa ya utawala na madaraka.
Ingawa Mapapa kwa kawaida hawataji majina ya viongozi, Papa Leo XIV amevunja mwiko huo hivi karibuni. Wiki iliyopita, alimzungumzia Trump moja kwa moja akisema anatumaini Rais huyo anatafuta "njia ya kutokea" ili kumaliza vita. Kauli hizi zinakinzana na matamshi ya mmoja wa viongozi wa Marekani, Pete Hegseth, ambaye alitaja vita vya Iran kuwa "vita vitakatifu" na kuomba "nguvu kubwa ya kijeshi dhidi ya wasiostahili rehema."
Akijibu msimamo huo wa utawala wa Trump, Papa alikariri maneno ya Biblia akisema: "Hata mkiomba maombi mengi, sitasikiliza; mikono yenu imejaa damu," akiongeza kuwa Mungu hasikilizi sala za wale wanaopigana vita.
Mvutano kati ya Vatican na Ikulu ya Marekani ulianza tangu mwaka jana wakati Leo alipokosoa madai ya Makamu wa Rais, JD Vance, kuhusu wahamiaji.
Katika kile kinachoonekana kama dharau ya kidiplomasia, Papa amekataa mwaliko wa Vance wa kutembelea Marekani mnamo Julai 4 (Siku ya Uhuru wa Marekani), na badala yake amepanga kutembelea kisiwa cha Lampedusa nchini Italia kuwafariji wahamiaji wanaotokea Afrika.
Hii ni Pasaka ya kwanza kwa Papa Leo XIV tangu kuchaguliwa kwake mwezi Mei mwaka jana, kufuatia kifo cha Papa Francis aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Post a Comment