TFF Kutia Mkazo Sheria Wachezaji wa Kigeni Kulinda Viwango
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuwa msimu huu litaweka mkazo mkubwa katika utekelezaji wa Kanuni ya 62 (4)inayotaka wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa nchini kuwa ni wale tu wenye sifa ya kuchezea timu za taifa za nchi zao.
Rais wa TFF, Wallace Karia alifunguka hayo katika mahojiano maalumu na gazeti la HabariLEO na kuweka wazi kuwa kipengele hicho siyo kigeni kwenye vitabu vya sheria, bali kilikuwa hakitiliwi mkazo huko nyuma.
Amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti uingizaji wa wachezaji wa viwango vya chini ili kukuza ushindani wa kweli.
Karia alibainisha kuwa lengo kuu la sheria hiyo ni kuhakikisha ligi inapata wachezaji wenye kiwango kikubwa na soka la ushindani linaloweza kusaidia wachezaji wazawa kujifunza na kukua kisoka.
Alikiri kuwa huko nyuma utekelezaji wake ulikabiliwa na changamoto kutokana na mwanya ulioruhusu mchezaji wa kigeni kusajiliwa mradi tu anatokea klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi yake au kwingineko duniani, lakini akasisitiza kuwa zama hizo za mazoea zimefika mwisho na sasa kigezo cha kucheza timu ya taifa ndio kitakuwa dira kuu.
Pamoja na mabadiliko hayo, TFF imethibitisha kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa kwa kila klabu itabaki kuwa 12 kama ilivyo sasa.
Karia alieleza kuwa idadi hiyo haitapunguzwa kwa sababu uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni wenye sifa na viwango bora tayari umethibitika kusaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha ushindani na mbinu miongoni mwa wachezaji wazawa wanaopambana nao kupata namba kikosi cha kwanza.
Upande wa walinda mlango, shirikisho hilo limesimamia kidete Kanuni ya 62 Kipengele cha 1.2 kinachozuia klabu kusajili zaidi ya golikipa mmoja wa kigeni kwa ajili ya mashindano yote yaliyo chini ya TFF.
Rais Karia alifafanua kuwa sheria hii imewekwa kimkakati ili kulinda makipa wazawa na kuwapa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye klabu zao, hatua ambayo ni mwarobaini wa kutatua uhaba wa makipa bora wenye viwango vya ushindani wa kimataifa pindi wanapoitajika kuitumikia timu ya taifa ya ‘Taifa Stars’.
Sambamba na masharti hayo ya kikanuni, klabu zitakazokusudia kusajili nyota wa kigeni zitatakiwa kujipanga kifedha ambapo ada ya usajili imewekwa kuwa Shilingi milioni nane kwa kila mchezaji mmoja.

Post a Comment