MUDA WA KUPOKEA KAZI ZA TUZO ZA SAMIA KALAMU WAONGEZWA SIKU 14

 


KAMATI ya Maandalizi ya Mashindano ya Samia Kalamu Awards (SKA) 2026, imetangaza kuongeza muda wa kupokea kazi za kushindanishwa kwa siku kumi na nne (14) zaidi, ili kutoa fursa kwa wadau wengi wa sekta ya habari na utangazaji nchini kushiriki kikamilifu.

Nyongeza hiyo ya muda inaanza rasmi leo tarehe 1 Julai 2026 hadi tarehe 14 Julai 2026 saa 5:59 usiku, tofauti na ratiba ya awali ambayo ilionyesha kuwa mwisho wa kupokea kazi hizo ilikuwa tarehe 30 Juni 2026. Hatua hiyo imefikiwa kufuatia maombi mengi yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali wa habari nchini walioomba kuongezewa muda ili kukamilisha maandalizi ya kazi zao.

Viongozi wakuu wa kamati hiyo, Mwenyekiti Mhandisi Peter P. Mwasalyanda na Mwenyekiti Mwenza Daktari Rose Reuben, wamewahimiza waandishi wa habari, wahariri, wachora katuni, maafisa habari, na watengeneza maudhui ya kidijitali kutumia vyema fursa hiyo. Wamesema kuwa maelezo yote kuhusu makundi ya tuzo na vigezo vya ushiriki yanapatikana kwenye tovuti yao rasmi ya samiaawards.tz.

Tuzo za Samia Kalamu Awards zilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kutambua na kuhamasisha ubora na ubunifu katika uandishi wa habari za maendeleo. Mashindano haya yanaratibiwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), yakiwa na kaulimbiu ya “Kalamu kwa Maendeleo” inayolenga kuimarisha taswira chanya ya nchi.

No comments