Watanzania wapasua mashindano ya hisabati Afrika



Tanzania imeendelea kujiyakulia heshima kubwa katika ulimwengu wa kitaaluma baada ya wanafunzi sita wa shule za sekondari nchini kunyakua jumla ya medali tisa katika Mashindano ya Hisabati ya Afrika yaliyofanyika nchini Ivory Coast. 

Katika mtihani huo mzito wa akili, timu ya Tanzania ilifanikiwa kuweka rekodi mpya kwa kushika nafasi ya tano kati ya nchi 26 zilizoshiriki barani kote, ikionyesha maendeleo makubwa ukilinganisha na mwaka 2025 ambapo nchi ilishika nafasi ya 10. 

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), Dk. Said Sima, pichani, alibainisha jijini Dar es Salaam kuwa ushindi wa mwaka huu umepasua anga baada ya wasichana watatu kuvuna medali mbili kila mmoja, huku wavulana watatu wakiondoka na medali moja kila mmoja, mafanikio yanayozidi kuikuza Tanzania kama kinara wa somo hilo ikizingatiwa ilitwaa medali nne mwaka 2024 na idadi kama hiyo mwaka jana.

Wataalamu hao wachanga wa mahesabu waliofanya maajabu nchini Ivory Coast walipatikana baada ya kuchujwa kwa umakini mkubwa kupitia majaribio matatu ya tathmini, yaliyofuatia Mashindano ya Hisabati ya Tanzania (TAMO) yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana. 

Katika mchanganuo wa ushindi huo wa kihistoria, medali za shaba katika kipengele cha jumla zilikwenda kwa Angel Zalwango wa Shule ya Sekondari White Lake, Sweetbert Nene wa Ilboru, na Nyandahu Leonard wa Shule ya Sekondari Kibaha. 

Nazo medali za fedha zilinyakuliwa na Lightness Ngiliule wa St. Francis, Joyce Sulumo wa Kilakala, pamoja na Arqam Salim wa Shule ya Rehema Wakfu. 

Ushindi huo ulikwenda mbali zaidi baada ya wasichana wetu kutakata kwenye kipengele maalumu cha wanawake, ambapo Lightness aliondoka na medali ya dhahabu, Joyce akatwaa fedha, na Angel akahitimisha kwa medali ya shaba, mafanikio yanayothibitisha mchango mkubwa wa CHAHITA tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966 katika kukuza ufundishaji na ujifunzaji wa hisabati nchini.

Baada ya kuitingisha Afrika, vijana hawa sita sasa wanajiandaa kupeperusha bendera ya Taifa katika Mashindano ya Kimataifa ya Hisabati ya mwaka 2026 yatakayofanyika jijini Shanghai, nchini China kuanzia Julai 10 hadi 21 mwaka huu. 

Kufuatia hatua hiyo kubwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Peter Mwasalyanda, amewapongeza vijana hao kwa kuiletea nchi sifa na kueleza kuwa TCRA ilifadhili ushiriki huo kama sehemu ya mkakati wake wa kukuza masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STUH).

 Mwasalyanda alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu nchini kujiunga na kuunda vilabu vya kidijiti, hatua itakayosaidia kukuza ujuzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuwajengea uelewa mpana wa masuala ya kidijiti ili waweze kushindana kikamilifu katika soko la sasa la ulimwengu.

No comments