DC MPOGOLO AWAKANYA ASKARI WA AKIBA DHIDI YA UBABE NA UONEVU
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka askari wa Jeshi la Akiba waliopangiwa kazi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kusimamia maadili ya kazi na kuzingatia sheria ili kuepuka kuwa kero kwa wananchi.
Akitoa maelekezo na mwongozo wa kiutendaji kwa askari hao mwishoni mwa wiki, Mpogolo alisisitiza kuwa utendaji wao unapaswa kuongozwa na busara badala ya kutumia nguvu kupita kiasi, akisema kuwa wanapaswa "kutumia akili nyingi na nguvu kidogo" katika kutekeleza majukumu yao.
Mpogolo alionya vikali dhidi ya askari hao kutumiwa na viongozi wasio waadilifu kwa maslahi binafsi, hususan katika ukusanyaji wa fedha kinyume cha taratibu. Aliwataka askari hao kuwa na msimamo na kutokubali maelekezo yanayokiuka maadili ya kazi zao, akibainisha kuwa uadilifu unajengwa kwa kusimamia miiko na kutambua mipaka ya madaraka.
Aliongeza kuwa askari anayezingatia maadili anapaswa kujua ni agizo gani la mkuu wake ni halali na lipi linalolenga kudhulumu mali za watu.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alikumbusha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeundwa kisheria na si kwa matakwa ya mtu binafsi, hivyo utendaji wa askari hao lazima uakisi misingi hiyo ya kisheria.
Aliwataka kuhakikisha hawi wababe wala waonevu kwa wananchi, bali wawe walinzi wa taratibu zilizowekwa na Mkurugenzi wa Jiji ambazo zimekuwa zikitangazwa mara kwa mara kuwakumbusha wananchi wajibu wao.
Katika kuhitimisha maelekezo yake, Mpogolo alikumbusha kuwa takriban asilimia 96 ya wakazi wa Dar es Salaam wanategemea biashara kama chanzo chao kikuu cha mapato. Kutokana na ukweli huo, aliwataka askari wa akiba kutengeneza mazingira salama yatakayowawezesha wananchi kutafuta riziki zao bila kuathiri watumiaji wengine wa jiji.
Alisisitiza kuwa lengo ni kuwa na utaratibu wa kibiashara unaozingatia usalama na amani, badala ya kujenga uhusiano wa hofu kati ya askari na wafanyabiashara.

Post a Comment