KATIBU MKUU WA CAF NA NCHI WENYEJI WAKUTANA KUJADILI MAANDALIZI YA AFCON 2027



Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika  (CAF), Bw. Samson Adamu, amefanya kikao maalum na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma, pamoja na Waziri wa Michezo wa Kenya Mhe. Salim Mvurya, Waziri wa Michezo wa Uganda Mhe. Peter Ongoing, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda, ambapo kwa pamoja wamejadili hatua mbalimbali za maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027.

Katika kikao hicho kilichofanyika Aprili 23, 2026 Kampala Uganda, viongozi hao wamepitia masuala muhimu yanayohusu maandalizi ya miundombinu, uratibu wa kamati za maandalizi, usalama, pamoja na mikakati ya kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanyika kwa viwango vya kimataifa.






Mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za pamoja za Tanzania, Kenya na Uganda, nchi wenyeji wa mashindano hayo, katika kuhakikisha AFCON 2027 ambayo inatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 18, 2027 inafanikiwa na kuwa miongoni mwa mashindano bora zaidi kuwahi kufanyika barani Afrika.

Aidha, mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya AFCON (Tanzania) Bw. Leodgar Tenga, pamoja na Marais wa mashirikisho ya mpira wa miguu wa mataifa wenyeji; Bw. Wallace Karia (Tanzania), Bw. Moses Magogo (Uganda), na Bw. Hussein Mohamed (Kenya).

No comments