RAIS SAMIA APOKEA RIPOTI YA TUME YA UCHUNGUZI; WITO WA UPONYAJI,UWAJIBIKAJI NA MAREKEBISHO YA KITAIFA WATOLEWA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan, leo amepokea rasmi Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza
Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 2025.
Tukio hili linaashiria
mwanzo wa hatua ya utekelezaji wa mapendekezo ya kuponya Taifa, kuimarisha
uwajibikaji na kujenga mustakabali imara zaidi.
Akizungumza wakati wa kupokea ripoti hiyo, Mheshimiwa Rais
alitambua kwa uzito mkubwa madhara yaliyolikumba Taifa, akipokea maelezo kuwa
matukio hayo yalisababisha vifo vya takribani watu 518, majeruhi zaidi ya
2,390, na uharibifu wa mali unaokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 125.
Alisisitiza kuwa hasara hizi zimeacha majeraha makubwa ya kijamii, kiuchumi na
kisaikolojia kwa wananchi.
“Hili ni janga na doa kubwa kwa Taifa letu.” Alisema Rais
Dkt. Samia.
Mheshimiwa Rais alieleza kuwa kazi ya Tume imeiwezesha nchi
kupata uelewa sahihi wa kilichotokea, ikijumuisha uchambuzi wa kina uliotokana
na ushahidi wa mashahidi 1,323, maelezo ya viapo 953, pamoja na maoni
yaliyokusanywa kupitia njia mbalimbali ikiwemo zaidi ya ujumbe mfupi 33,000 na
maoni ya maelfu ya wananchi katika maeneo 202 yaliyofanyiwa uchunguzi.
“Wakati mwingine dawa ni chungu, lakini kama tunataka
kupona, lazima tunywe dawa. Tume imechunguza kilichotusibu. Kazi yetu sasa ni
kutumia dawa hiyo ipasavyo,” amesema Rais Dkt. Samia na kusisitiza kuwa Taifa
lina wajibu wa kuhakikisha matukio hayo hayajirudii kwa kuchukua hatua za
marekebisho na uwajibikaji.
Aidha, Mheshimiwa Rais alihimiza mshikamano wa kitaifa
akibainisha kuwa mustakabali wa nchi uko mikononi mwa Watanzania wenyewe.
“Hatma ya Tanzania ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe.”
Katika juhudi za kuliponya Taifa, alitoa wito mahsusi kwa
viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maridhiano na
kurejesha maadili ya jamii.
“Simamieni nafasi yenu ya kuliponya Taifa letu.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu Mstaafu
Mohamed Chande Othman, alisema kuwa Ripoti hiyo ni matokeo ya uchunguzi mpana
uliodumu kwa siku 153, ukihusisha mikoa 11, wilaya 21, na maeneo 202
yaliyoathirika zaidi. Alieleza kuwa mchakato huo ulihusisha pia mijadala ya
vikundi zaidi ya 200 na ushirikishwaji mpana wa wananchi.
“Ripoti tunayoiwasilisha inabeba dhamira ya pamoja ya Taifa
ya kutibu majeraha, kuwajibika kila panapostahili, lakini muhimu zaidi
kujifunza na kusonga mbele,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume na kuongeza kuwa, licha ya maumivu
makubwa yaliyosikika kutoka kwa waathirika, Watanzania wengi walionesha utayari
wa kushiriki katika safari ya maridhiano na kujenga upya mshikamano wa kitaifa.
“Waliowasiliana na Tume walionesha wazi kuwa yaliyotokea
siyo taswira halisi ya Utanzania wetu.”
Mheshimiwa Rais alikiri uzito wa jukumu lililopo mbele yake
na kuahidi kulibeba kwa ujasiri huku akihimiza ushirikiano wa wote.
“Nataka niwahakikishie nitaubeba mzigo huu kwa ujasiri na
kujiamini na hadhari kubwa. Kwa pamoja tutafanya. Tusimuachie Samia peke yake.”
Katika hitimisho lake, Mheshimiwa Rais aliwataka Watanzania
kujifunza kutokana na yaliyotokea na kusonga mbele kwa umoja na dhamira mpya ya
kulijenga Taifa.
“Tumegusa kaa la moto, na tumejifunza,” alisema.
Hii ni Tume ya saba ya Rais ya Uchunguzi tangu Uhuru. Tume
iliundwa tarehe 18 Novemba, 2025 na kuanza kazi tarehe 20 Novemba, 2025. Tume
ilikuwa na wajumbe tisa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande
Othman.
Wajumbe wengine ni pamoja na Prof. Ibrahim Hamis Juma,
Balozi Ombeni Yohana Sefue, Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Bw. Said Ally Mwema,
Balozi George Kahema Madafa, Balozi Paul Meela, Balozi Radhia Naima Msuya na
Balozi David Joseph Kapya.
Tume ilikusanya ushahidi kutoka kwa maelfu ya wananchi
kupitia mbinu mbalimbali za kisayansi na kijamii ili kubaini ukweli wa matukio
na kutoa mapendekezo ya kuimarisha amani, uwajibikaji na mshikamano wa kitaifa.







Post a Comment