Kamati ya Bunge Yataka Vijana Kuchangamkia Fursa Kilimo cha Chai Mponde



Vijana nchini wameshauriwa kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye mnyororo wa thamani wa zao la chai ikiwemo kuanzisha mashamba  ili wawe na uhakika wa ajira na kipato.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii katika Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Akizungumza Machi 14, 2026 katika kiwanda hichi kinachomilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma - PSSSF na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi - WCF,Mwenyekiti wa kamati hiyo Hawa Mchafu, aliwahimiza vijana na wananchi wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la chai kutokana na uwepo wa soko la uhakika la zao hilo,Kiwanda cha Chai cha Mponde.

Kamati hiyo imeeleza kuwa kilimo cha chai  ni chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa vijana endapo watajitokeza kukitumia kikamilifu  kutokana na uwepo wa kiwanda kinachonunua na kuchakata zao hilo katika eneo hilo.

"Vijana wengi wanakimbia  zao hili la chai na kuwaachia wazee kufanya kazi hiyo, tunatamani kiwanda hiki kisipungukiwe malighafi, hivyo vijana wahamasishwe kwa wingi kuchangamkia fursa hii kwa sababu tunalo soko la uhakika hapa Mponde"

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Mchafu, akizungumza baada ya kamati yake kukamilisha kutembelea kiwanda.




Awali akizungumza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano  Deus Sangu amesema kiwanda hicho kinauza chai zake katika masoko ya ndani na nje ya nchi kupitia wanunuzi ndani, minada ya chai pamoja na mikataba ya moja kwa moja.

Waziri Sangu amesema katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 kiwanda kiliuza kilo 220,762 za chai na kuingiza mapato ya takribani Tshs Milioni 779.

Katika hatua nyingine, amesema kiwanda hicho kinanufaisha zaidi ya wakulima 3,500 wa zao la chai na kutoa ajira za kudumu 79, Ajira za muda kati 100 hadi 300 kutegemea na msimu wa mavuno.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Muhoja Manane amesema kiwanda kitaendelea kujiimarisha na kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa ili kuwavutia wawekezaji na kujitambulisha katika soko la kimataifa.

Kamati hiyo inaendelea na ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi ,Ajira na Mahusiano na taasisi zake za PSSSF, WCF,NSSF na CMA.

No comments