MAANDALIZI AFCON: MPOGOLO AHAMASISHA UPAKAJI RANGI NA AFYA
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema kuwa kuelekea mashindano hayo, Wilaya ya Ilala ambayo ndiyo lango kuu la nchi na kitovu cha shughuli za kiserikali na kiuchumi, itahakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote na miundombinu ya afya inaimarishwa kukabili ongezeko la watu.
Akizungumza kwenye kikao kazi na Kamati ya Afya ya Msingi, Mpogolo amebainisha kuwa Serikali imejipanga vizuri kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 7 kwa ajili ya maboresho ya kituo cha afya Mchikichini, sambamba na kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ilala Mnazi mmoja ili kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana kwa ufanisi.
"Tunaelekea kwenye uenyeji wa AFCON. Halmashauri yetu ndiyo kioo, nembo, na lango la kuingilia Tanzania. Sisi ndio katikati ya jiji na hapa ndipo ilipo Ikulu. Tunaboresha mazingira ya afya yawe safi siku zote ili maeneo yote yawe imara na bora kwa ajili ya wakazi wetu na wageni watakaoingia," alisema Mpogolo.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa wakazi wa Ilala na wamiliki wa majengo kupaka rangi nyumba zao ili kuongeza urembo na mvuto wa mji. Alisisitiza kuwa ni jambo la kawaida na la kistaarabu kufanya maboresho ya muonekano wa majengo, hasa kuelekea tukio kubwa kama AFCON ambalo litailetea nchi heshima kubwa duniani.
Katika hatua nyingine, Mpogolo amesema jiji limeanza kampeni ya kuhamasisha Bima ya Afya kwa Wote, ikilenga kufikia watu milioni tatu wanaoingia na kutoka Ilala kila siku. Alisema maafisa watawafikia wananchi kwenye masoko makubwa kama Kariakoo, maeneo ya kibiashara, na vituo vya usafiri ikiwemo kwa madereva wa bodaboda na bajaji.
Maandalizi haya ya Ilala yanatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha kuwa uenyeji wa AFCON unakuwa fursa ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa huduma bora za afya, mazingira safi, na ukarimu uliotukuka kwa maelfu ya mashabiki wa soka watakaomiminika nchini.

Post a Comment