Tanzania yawa ‘Shule’ ya Uhifadhi na Utalii Afrika,waja kusaka siri ya mafanikio




Mafanikio makubwa ya Tanzania katika kuoanisha uhifadhi wa maliasili na ukuaji wa sekta ya utalii yameendelea kuvutia macho ya mataifa ya nje, ambapo ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Zambia umewasili nchini kwa ziara maalum ya mafunzo na kubadilishana uzoefu. 

Hatua hii ni kielelezo cha namna Tanzania ilivyopiga hatua katika diplomasia ya kiuchumi na usimamizi wa rasilimali, ikiacha nyuma kelele za wapotosha taswira na badala yake ikijikita katika matokeo yanayoonekana duniani.

Ujumbe huo wa Zambia, ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Baraza la Mawaziri nchini humo, Siazongo Siakalenge, umekuja nchini mahususi kujifunza mbinu na mikakati ambayo Tanzania inatumia kutekeleza uhifadhi wa rasilimali za asili huku ikitangaza vivutio vyake katika masoko ya kimataifa. 

Wataalamu hao wamevutiwa na namna mifumo yetu ya usimamizi wa hifadhi na uendelezaji wa vivutio inavyofanya kazi kwa ufanisi mkubwa, jambo ambalo limeifanya nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuvutia watalii duniani.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya ujumbe huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, amebainisha kuwa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kuunganisha juhudi za uhifadhi na maendeleo ya utalii kwa namna inayochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa. 

Mafuru amesisitiza kuwa mfumo imara wa masoko ya kimataifa na uwekezaji kwenye miundombinu ya utalii ndiyo siri inayozidi kupaisha jina la Tanzania kila uchao.

Ziara hii ya wataalamu wa Zambia ni ushindi mwingine wa kishindo kwa nchi yetu, ikithibitisha kuwa uelekeo wa serikali katika kusimamia maliasili uko salama na unaaminika kimataifa. 

Wakati mataifa mengine yakija kuchota maarifa kwetu, ni wazi kuwa "visokorokwinyo" na wachafuzi wa hali ya hewa hawana nafasi mbele ya ukweli wa mafanikio haya yanayozidi kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii na uhifadhi barani Afrika.


No comments