SERIKALI YA MWINYI YAFUTA MIRADI, VISIWA VYA UWEKEZAJI KWA KUSUASUA
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetuma salamu nzito kwa wawekezaji wanaochukua maeneo na kushindwa kuyaendeleza, baada ya kutangaza kufuta miradi mitano ya uwekezaji na kuvinyang’anya visiwa sita wawekezaji waliozembea kuanza utekelezaji ndani ya muda uliopangwa.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa msimamo thabiti wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Rais Dk. Hussein Mwinyi, inayosisitiza kuwa Zanzibar si shamba la bibi na haitavumilia mchezo wala hadaa kutoka kwa wawekezaji wasiofuata makubaliano na ratiba za kazi.
Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff, amebainisha kuwa visiwa vingine viwili vipo kwenye hatari ya kufutiwa uwekezaji muda wowote kuanzia sasa iwapo wamiliki wake hawatabadilika.
Waziri Shariff amesisitiza kuwa ukaguzi wa mara kwa mara utaendelea kufanyika ili kuhakikisha kila kipande cha ardhi kilichotolewa kinatumika kwa manufaa ya uchumi wa Wazanzibari, huku akionya kuwa cheti cha uwekezaji si tiketi ya kumiliki ardhi bila kuifanyia kazi.
Licha ya hatua hizo za kinidhamu, mazingira ya uwekezaji visiwani humo yameendelea kushamiri ambapo katika kipindi cha siku 100 pekee, Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imesajili miradi mipya 45 yenye thamani ya Sh bilioni 568. Ongezeko hilo linafanya jumla ya miradi iliyosajiliwa tangu Dk. Mwinyi aingie madarakani kufikia 607, ikiwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.9, hali inayochochea ukuaji wa uchumi endelevu na kuimarisha imani ya wawekezaji wa ndani na nje.
Katika kuelekea Mapinduzi ya Viwanda, miradi saba mikubwa ikiwemo viwanda vya nguo, chakula cha mifugo, uzalishaji wa kuku na hoteli za fahari imeanza ujenzi au kuwekewa mawe ya msingi, hatua iliyoingiza nchini takribani Shilingi trilioni 1.1 na kuzalisha ajira 2,767 kwa wananchi.
Aidha, SMZ imeanza mchakato wa kuandaa Sheria ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) itakayowalazimisha wawekezaji kuhakikisha jamii zinazozunguka miradi yao zinapata faida za moja kwa moja kupitia huduma za kijamii na kiuchumi.
Ili kuondoa urasimu na mianya ya ufisadi, ZIPA imekamilisha mfumo wa kidijitali uliounganishwa na taasisi 12, hali inayoongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato na kuharakisha utoaji wa huduma.
Sambamba na hayo, Serikali imejipanga kuwalipa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 10 wananchi wa maeneo ya Fumba, Dimani na wale waliopisha ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa mchezo wa gofu, huku ikihakikisha taratibu zote za kisheria zinazingatiwa ili kulinda haki za raia na kukuza diplomasia ya kiuchumi.

Post a Comment