DAR ES SALAAM YAMWAGA SSEBO: MWILI KUZIKWA KAYUNGA, UGANDA MACHI 17
JIJI la Dar es Salaam limetawaliwa na simanzi wakati wa hafla ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji na Biashara wa vituo vya EFM na TVE, Dennis Busulwa, maarufu kama ‘Ssebo’.
Tukio hilo lililongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, limehusisha viongozi wa Serikali, wadau wa habari, na mamia ya wananchi waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho.
SALAMU ZA RAIS SAMIA
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Makonda amekitaja kifo cha Ssebo kama pigo kubwa kwa tasnia ya habari nchini.
Amesema Rais ameguswa na mchango wa marehemu na amewasilisha rambirambi zake kwa familia, mke, na mtoto, kupitia kwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Makonda alimuelezea Ssebo kama mwanataaluma aliyewagusa wengi kwa ubunifu na utendaji wake uliotukuka.
ALAMA YA AFRIKA MASHARIKI
Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Fred Mwesigye, amebainisha kuwa Ssebo alikuwa kielelezo cha mshikamano wa Afrika Mashariki.
Marehemu aliishi Tanzania kwa takribani miaka 36 tangu alipokuja masomoni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na kufanikiwa kujenga urafiki na undugu wa kudumu kiasi cha wengi kutofahamu asili yake.
Mkurugenzi wa EFM, Francis Sizza ‘Majizzo’, amemuelezea marehemu kama mhimili mkuu aliyesaidia kufanikisha ndoto za kituo hicho.
Naye Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, na Mkurugenzi wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, walisisitiza kuwa jina "Ssebo" (lenye maana ya bwana mwenye heshima kwa Kiganda) lilienda sambamba na busara alizozionyesha maishani mwake.
SAFARI YA MWISHO: KUELEKEA LUGANZI
Baada ya kukamilika kwa hafla hiyo ya kuaga jijini Dar es Salaam, mwili wa Ssebo unatarajiwa kusafirishwa Machi 15, 2026, kuelekea nchini Uganda.
Ratiba ya mazishi inaonyesha kuwa mwili utapelekwa Namengo, Luganzi ambapo utalala nyumbani kwa mama yake mzazi kwa ajili ya maombolezo.
Machi 16, maombolezo yataendelea kijijini hapo kabla ya safari ya mwisho kuelekea Kayunga, Luganzi, ambako ndiko Dennis Busulwa 'Ssebo' atakapopumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Machi 17, 2026.
Post a Comment