VIJANA WAHITIMU WA KIGAMBONI WAANZA KUNG’ARA KATIKA MAKAMPUNI MAKUBWA NCHINI
Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini imeanza kuonyesha matokeo ya dhahiri kwa vitendo baada ya idadi kubwa ya vijana waliopata mafunzo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kigamboni kufanikiwa kupata ajira katika makampuni makubwa na taasisi za kimkakati hapa nchini.
Mafanikio hayo yamethibitika kufuatia ufuatiliaji uliofanyika kwa wahitimu wa mwaka 2025, ambao walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na huduma na kupata ajira hukohuko.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mheshimiwa Deus Sangu, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa programu ya taifa ya kukuza ujuzi katika chuo cha maendeleo ya wananchi Kigamboni Dar es salaam kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na maendeleo ya Jamii iliyo chini ya Mbunge Hawa Mchafu.
Katika taarifa yake hiyo Waziri Sangu alisema vijana hao sasa wameajiriwa katika makampuni yenye hadhi ya juu yakiwemo Saturn Corporation, World Oil, Songolo Marine Transport, na Rose Designs. Aidha, wengine wamepata nafasi katika taasisi za huduma za jamii kama DAWASA, TANESCO, na kampuni za ujenzi na usafirishaji kama SBL Infrastructure na GTS Logistics.
Alisema kuajiriwa kwa vijana hao waliofika katika kampuni hizo kwa mazoezi inathibitisha kuwa ujuzi wanaoupata unakidhi mahitaji ya soko la ajira.
Aidha alisema katika kuelekea mwaka wa fedha 2025/26, Serikali imejipanga kuongeza nguvu katika programu hii ambapo tayari jumla ya Shilingi milioni 60 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia mafunzo katika Chuo cha Kigamboni. Katika kiasi hicho, tayari Shilingi milioni 30 zimeshatolewa kwa ajili ya awamu ya kwanza na ya pili ya malipo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mafunzo kwa vijana 120 waliochaguliwa kwa mwaka huu. Vijana hawa wanajumuisha wavulana 73 na wasichana 47, huku kundi la watu wenye ulemavu likipewa kipaumbele kwa kuwajumuisha vijana watano katika fani mbalimbali.
Mafunzo yanayotolewa yanagusa nyanja muhimu za kiufundi ambazo zina uhitaji mkubwa wa mafundi stadi, ikiwemo fani ya umeme wa majumbani na viwandani, ufundi wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, pamoja na ufundi bomba na ushonaji. Takwimu zinaonyesha kuwa fani ya umeme wa majumbani inaongoza kwa kuwa na wanafunzi 30, ikifuatiwa na ufundi wa magari wenye vijana 30, huku fani nyingine zikigawanywa kulingana na mahitaji na uwezo wa chuo.
Utekelezaji wa programu hii unalenga si tu kutoa ajira za mkataba, bali pia kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri wenyewe. Hadi sasa, baadhi ya wahitimu wameonyesha mfano wa kuigwa kwa kuanzisha shughuli zao binafsi, hatua inayosaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi kuanzia ngazi ya jamii. Serikali imesisitiza kuendelea kuwasimamia vijana hawa ili kuhakikisha wanatumia fursa hiyo adhimu kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa chuo hicho cha Kigamboni, Mhandisi Ramadhani Simba amesema tangu kuanza utekelezaji wa Programu ya Uanagenzi (Apprenticeship) chuoni hapo kumekuwa na mafanikio makubwa.
Alisema Chuo kimefanikiwa kuwa kitovu cha mafunzo ya vitendo ambapo vijana huchukua miezi sita kupata ujuzi, wakitumia asilimia 80 ya muda wao viwandani. Katika awamu ya saba (2025), vijana 155 walihitimu, na kwa mwaka huu wa 2026, wanagenzi 120 (akiwemo vijana 5 wenye ulemavu) wanaendelea na mafunzo katika fani za umeme, ufundi magari, uchomeleaji, ufundi bomba, na ushonaji.
Aidha Mhandisi Simba amesema kwamba Chuo hicho kinatekeleza programu ya "Elimu Haina Mwisho" (EHM), inayowasaidia mabinti waliokatisha masomo (ikiwemo sababu ya ujauzito) kurejea kwenye mfumo wa elimu na teknolojia. Pia, kuna programu ya "Mpira Fursa" inayolenga kuibua vipaji vya michezo na ufundi kwa vijana kuanzia ngazi ya shule za msingi.
Chuo hicho kwa sasa kimekamilisha ujenzi wa hosteli yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 320, jambo lililosaidia kuongeza udahili wa vijana kutoka maeneo mbalimbali. Pia, chuo kimeimarisha mashirikiano na taasisi kama BRELA na TRA ili kuwafunza vijana masuala ya biashara na kisheria.
Kamati hiyo ya bunge pamoja na kutoa mapendekezo kadhaa ya uboreshaji wa mafunzo hasa utoaji wa mitaji baada ya mafunzo, wamepongeza hatua iliyochukuliwa na serikali katika kuhakikisha taifa linakuwa na nguvu kazi yenye stadi zinazoshindana sokoni.
Aidha wameitaka serikali kutanua wigo wa udahili ambao kwa sasa hata nusu ya uwezo wa vyuo nchini haujafikiwa. Vyuo vya ufundi nchini vina uwezo wa kupokea wananchi elfu 16 lakini waliopata nafasi kwa sasa ni zaidi ya 5000.
Post a Comment