Maji ni Salama: Kunenge akata mzizi wa fitina
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa kauli nzito inayolenga kuondoa hofu kwa wananchi kufuatia uvumi na propaganda zisizo na msingi zinazoenezwa na baadhi ya watu kuhusu usalama wa miundombinu ya maji.
Akizungumza Machi 17, 2026, katika ziara ya mafunzo kwa madiwani kwenye mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini, na Wami, Kunenge amesisitiza kuwa mfumo wa maji wa nchi yetu ni salama na hauwezi kuingiliwa au kuwekwa sumu kirahisi kama inavyovumishwa na wachafuzi wa taswira ya taifa kwenye mitandao ya kijamii.
Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika ulinzi wa kisasa na teknolojia inayofuatilia vyanzo na mitambo ya uzalishaji maji kwa saa 24, jambo linalofanya maji yanayowafikia wananchi kuwa safi na salama wakati wote.
Kunenge amewataka wananchi kupuuza kelele za watu wanaotafuta taharuki na badala yake waendelee kuiamini mifumo rasmi ya serikali. Aidha, amewataka madiwani na viongozi wa jamii kuacha malalamiko yasiyo na suluhisho na badala yake wawe daraja la kuelimisha umma kuhusu juhudi kubwa zinazofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) katika kuhudumia mamilioni ya wakazi wa Pwani na Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, mkazo mkubwa umewekwa katika utunzaji wa mazingira kama njia pekee ya kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.
Kunenge amerejea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kulinda vyanzo vya maji dhidi ya ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kilimo holela kando ya mito.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa DAWASA, Eng. Mkama Bwire, serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pampu mpya na uboreshaji wa mitambo ya Ruvu ili kuziba pengo la mahitaji ya maji ambayo yameongezeka kufikia lita milioni 772 kwa siku.
Hatua hizi za kimkakati ni uthibitisho kuwa serikali iko kazini na usalama wa mwananchi ni kipaumbele cha kwanza, hivyo kelele za "wachafuzi" hazipaswi kupewa nafasi ya kubomoa imani hiyo.

Post a Comment