VIJANA WA KITANZANIA SASA WAUNDA VICHWA VYA TRENI
Katika kile kinachoonekana kuwa ni mapinduzi makubwa ya teknolojia na uzalendo, juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwezesha ufundi kwa vijana zimeanza kulipa kwa kishindo kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuandika historia mpya kwa kufanikiwa kuunda na kukarabati vichwa vya treni za reli ya zamani (MGR - Meter Gauge Railway) katika karakana ya Pugu.
Meter Gauge Railway (MGR) ni reli ya zamani ya mita moja ambayo imekuwepo nchini kwa miaka mingi, tofauti na reli mpya ya kisasa ya SGR (Standard Gauge Railway).
Hatua hiyo inathibitisha kuwa uwekezaji kwa vijana wa Kitanzania ndio mkombozi wa uchumi wa taifa.
Imeelezwa kuwa vichwa viwili vya treni kati ya vinane vya daraja la 91XX vimeundwa katika karakana ya TRC iliyopo Dar es Salaam kupitia mradi wa uundaji wa vichwa vya treni za MGR.
Akizungumza baada ya kukagua karakana hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso aliitaka Wizara ya Uchukuzi kupitia TRC kuendelea kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania wanaohusika katika uundaji na ukarabati wa vichwa hivyo kwa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa uamuzi wa TRC kuanza kuunda vichwa vya treni hapa nchini umeipunguzia serikali gharama ambazo zingetumika kununua vifaa hivyo nje ya nchi, huku pia ukitoa ajira kwa vijana na kuwapa nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibwa Shiwa alisema kuanza uundaji wa vichwa vya treni nchini utapunguza muda na gharama za kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.Aliongeza kuwa TRC ina mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi ili kuweza kuunda vichwa takribani 30 kwa mwaka, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi na kuhakikisha upatikanaji wa vichwa vya treni kwa wakati.
Aidha Shiwa, amebainisha kuwa mradi huo wa uundaji wa vichwa vya daraja la 91XX umetoa ajira kwa vijana 34 ambao hapo awali walikuwa mitaani. Aidha, mradi umekuwa kichocheo cha biashara kwa wazawa wanaouza bidhaa kama vifaa vya umeme, bolti, nati, na vilainishi, hivyo kukuza mnyororo wa thamani wa ndani.

Post a Comment