VIJANA, MAKAMPUNI YA WAZAWA WAVUNA TRILIONI 3.8 SEKTA YA MADINI




Kampuni za Kitanzania, zikiwemo zile zinazoongozwa na vijana, zimefanikiwa kuingiza jumla ya Sh trilioni 3.8 kupitia utoaji wa bidhaa na huduma katika migodi mbalimbali nchini ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita. 

Mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), ambapo Tume ya Madini imetenga bidhaa na huduma 20 maalum ambazo zinatolewa na kampuni za kizalendo pekee zenye umiliki wa asilimia 100, hatua inayolenga kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi kiuchumi.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Hamis Kamando, amebainisha kuwa katika kipindi hicho cha Julai hadi Desemba 2025, sekta hiyo imepiga hatua nyingine kubwa kwa kuongeza thamani ya madini yenye thamani ya Sh trilioni 5.8 hapa nchini. 

Hatua hii imesaidia kuzuia usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje na badala yake kutengeneza fursa za ajira 273 katika viwanda saba vya uchenjuaji na uongezaji thamani vilivyopo nchini, ambapo asilimia kubwa ya waajiriwa hao ni vijana wa Kitanzania waliopewa kipaumbele.

Ili kuendeleza kasi hiyo ya ushiriki wa wazawa, Tume ya Madini imeingia makubaliano ya kihistoria na Benki ya CRDB kupitia Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa Februari 23, 2026, kwa lengo la kutatua changamoto ya mitaji. 

Ushirikiano huo unalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo, hususan vijana, kupata mikopo na uwekezaji utakaowawezesha kununua vitendea kazi vya kisasa na kuongeza tija katika shughuli zao, jambo ambalo limekuwa likiwakwamisha kwa muda mrefu.

Mbali na nyanja ya kifedha, Serikali kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo 579 katika mikoa ya Geita, Mbogwe, na Chunya.

Mafunzo hayo yamejikita katika kuwajengea uwezo vijana kuhusu umiliki wa leseni, usimamizi wa maduara, na biashara ya madini ili kuhakikisha wanashiriki katika mnyororo mzima wa thamani kwa weledi na tija, badala ya kubaki kuwa vibarua tu katika sekta hiyo.

Kwa sasa, viwanda vya uongezaji thamani kama Mwanza Metals Refinery na Geita Gold Refinery vimekuwa kielelezo cha namna wataalamu wazalendo wanavyoweza kuendesha mitambo ya kisasa. Kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kituo cha Jeolojia (GST), Tume ya Madini imedhamiria kuendelea kutoa mafunzo ya teknolojia mpya ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya soko la dunia, ikihakikisha kuwa rasilimali za madini zinakuwa chachu ya kuondoa umaskini na kukuza pato la taifa kupitia nguvu kazi ya vijana.

No comments