BILIONI 200 ZA VIJANA: WADAU WATAJA SIRI YA KUFANIKIWA, WAONYA ‘MITEGO’ YA MIKOPO


Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Ahmmed Kitara,


Wakati Serikali ikimwaga takribani Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya kifursa kwa vijana nchini, wadau wa maendeleo na uchumi wameibuka na kutoa mwongozo wa namna ya kunusuru fedha hizo zisipotee kutokana na dhana potofu na ukosefu wa elimu ya biashara.

Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Ahmmed Kitara, amebainisha kuwa kikwazo kikubwa kwa vijana siyo upatikanaji wa fedha, bali ni ukosefu wa elimu sahihi na ushauri wa kitaalamu. Alisema vijana wengi huomba mikopo kwa kufuata mkumbo bila kuwa na ujuzi wa kutosha wa miradi wanayopendekeza.

“Mazungumzo na tathmini ya kina kati ya taasisi za fedha na waombaji mikopo husaidia kubaini kama kijana ana ujuzi na uwezo wa kutekeleza mradi wake. Changamoto kubwa ni vijana kutokupatiwa elimu ya kutosha na ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kuendeleza mawazo yao ya miradi,” alisema Kitara wakati akichangia mada hiyo Machi 12, 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Abdul Nondo, ameashiria kuwa bado kuna ombwe kubwa kati ya kiasi cha fedha kilichotengwa na uhalisia wa maisha ya vijana. Alieleza kuwa asilimia 80 ya vijana nchini wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi, hivyo wanahitaji mifumo madhubuti ya uratibu na taarifa sahihi.

Nondo alihimiza uwajibikaji kwa viongozi wanaopaswa kuwahamasisha vijana kunufaika na fursa hizo za kiserikali.

Hoja nyingine nzito imetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya TAFEYOKO, Elvis Mkumbo, ambaye ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya vijana kutumia mikopo hiyo kutatua matatizo binafsi badala ya uwekezaji. 

Mkumbo alisema mara nyingi mkopo humkuta kijana akiwa na dhiki za kifedha, hali inayosababisha fedha hizo kumezwa na mahitaji ya nyumbani badala ya kuendeleza mradi.

“Kijana anatumia sehemu kubwa ya fedha kutatua changamoto zake binafsi, na inayobaki haitoshi kuendeleza wazo la biashara. Hali hii inasababisha miradi kushindwa kuzalisha na kuisababishia Serikali hasara badala ya kunufaika na marejesho,” alionya Mkumbo, huku akisisitiza umuhimu wa mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kijana kukabidhiwa fedha.

Wadau hao kwa pamoja wamekubaliana kuwa, ili mshindo wa bilioni 200 za Rais Samia ulete mapinduzi ya kweli, lazima kuwepo na ufuatiliaji wa karibu (monitoring), elimu ya uraia na fedha, na vijana wenyewe wabadili fikra kwa kuona mikopo hiyo kama mtaji wa biashara na siyo "mgao" wa bure.

No comments