FAMILIA YA MAGUFULI YAHIMIZA UMOJA KUENZI FALSAFA YA ‘RAIS WA WANYONGE’




Familia ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, imetoa wito kwa Watanzania kudumisha umoja, mshikamano na upendo kama nguzo muhimu ya kumuenzi kiongozi huyo aliyekuwa akijulikana kwa falsafa ya kutetea wanyonge.

Rai hiyo imetolewa na binti wa kiongozi huyo, Jesca Magufuli, wakati wa shughuli za matendo ya huruma zilizofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya miaka mitano tangu kifo chake kilichotokea Machi 17, 2021.

Jesca, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (UVCCM) mkoani humo, amesisitiza kuwa undugu wa Watanzania unapaswa kudumishwa kwa kusaidiana katika vipindi vigumu, hususan kwa wale wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu na mahitaji ya msingi. 

Alibainisha kuwa kuwajali wasiojiweza ni njia bora ya kuishi maono ya baba yake, huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu na kuongeza vifaa tiba nchi nzima.

Katika ziara hiyo hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Madili Sakumi, alikiri kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya wagonjwa kumudu gharama, huku akimkumbuka Hayati Magufuli kwa kuipandisha hadhi hospitali hiyo kutoka kituo cha afya. 

Hata hivyo, uongozi wa hospitali umeomba Serikali kusaidia ukarabati wa uzio na nyumba za watumishi zilizochakaa, pamoja na kuhimiza wananchi kujitokeza kuchangia damu kutokana na uhaba wa akiba ya kutosha unaokabili kituo hicho.

Maadhimisho haya ya miaka mitano yamepambwa na mfululizo wa shughuli za kijamii na kiroho, ikiwemo mbio za asubuhi (jogging), uchangiaji damu, kutembelea wafungwa, na mkesha maalum wa kumbukizi. Shughuli hizi ni maandalizi ya kuelekea kilele cha kumbukizi hiyo ambapo Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuongoza viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, na viongozi wastaafu katika misa maalum nyumbani kwa marehemu.

Misa hiyo ya kumuombea na kumuenzi kiongozi huyo shupavu inatarajiwa kuongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi. 

Hayati Dk. Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kutokana na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, na tangu wakati huo amekuwa akisherehekewa kama kiongozi aliyeweka misingi imara ya uzalendo na maendeleo ya miundombinu nchini Tanzania.


No comments