WAZIRI MAKONDA ASIMAMISHA UCHAGUZI WA TOC, ATEUA KAMATI YA MUDA NA KUAGIZA UCHUNGUZI WA TAKUKURU
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, amesimamisha mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) uliokuwa ufanyike Aprili 12, 2026, sambamba na kuusimamisha uongozi wa sasa wa kamati hiyo.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko mazito kutoka kwa wagombea walioenguliwa, wakidai mchakato huo ulikosa uwazi, haki, na uwajibikaji, jambo lililozua taharuki miongoni mwa wadau wa michezo nchini.
Mheshimiwa Makonda amesisitiza kuwa, ingawa Serikali inaheshimu uhuru wa vyama vya michezo kulingana na misingi ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), uhuru huo haumaanishi taasisi ziendeshwe kinyume na utawala wa sheria na maslahi ya umma.
Waziri ametumia mamlaka yake kisheria chini ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49, akibainisha kuwa mchakato huo uligubikwa na sintofahamu iliyolenga kunufaisha watu wachache na kudhoofisha ustawi wa michezo nchini.
Katika hatua za kurekebisha hali hiyo, Waziri amemteua Ismail Aden Rage kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda (Interim Committee) akisaidiwa na Dkt. Steven Mabagala kama Makamu Mwenyekiti na Amina Mfaume kama Katibu. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Kesi Said Mohammed, Jemedari Said, Asma Hilal, na Queen Siraki, ambao watasimamia uongozi wa mpito wakati uchunguzi wa kina ukiendelea.
Sambamba na uongozi huo wa muda, Waziri Makonda ameagiza kuundwa kwa Kamati ya Uchunguzi itakayoshirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Kamati hiyo itachunguza tuhuma zote za ukiukwaji wa taratibu na mwenendo wa uchaguzi wa TOC ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika wote waliohusika kuvuruga misingi ya utawala bora.
Uamuzi huu wa Waziri, ambao ni wa mwisho kwa mujibu wa kifungu cha 27(2) cha Sheria ya BMT, unalenga kurejesha uadilifu na imani katika uongozi wa michezo.
Waziri amewahakikishia wadau kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira bora ya maendeleo ya michezo ili kuwezesha Tanzania kushinda medali za kimataifa, hususan za dhahabu, na amewaomba wadau kuwa watulivu wakati mchakato huu wa marekebisho ukikamilishwa kwa manufaa ya taifa.

Post a Comment