PROFESA CHIJORIGA AZUNGUMZIA CHACHU YA AMANI, UTULIVU NA MSHIKAMANO WA KITAIFA

 



Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS), Profesa Marcellina Chijoriga, amesisitiza kuwa huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kutafakari misingi ya umoja na utulivu iliyowekwa tangu uhuru mwaka 1961 ili kuhakikisha nchi inabaki kuwa salama kwa maendeleo ya wote.

Alisema hayo katika kongamano wa kuadhimisha kumbukizi ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere,  Dar es salaam leo.

Aliitaka jamii kutumia kongamano  hilo kukumbushia maisha ya kiongozi huyo kama dira ya kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.

“Amani na utulivu tulionao leo ni matokeo ya misingi imara ya uadilifu na uzalendo ambayo Mwalimu Nyerere alisimamia kwa dhati wakati wa uongozi wake” alisema  Profesa Chijoriga ambaye pia alibainisha kuwa urithi huo si wa kihistoria pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania wa kizazi hiki kuuendeleza kwa vitendo.

Ili kuendelea kuwa na taifa lenye mshikamano, alisema ni muhimu kuzingatia ulinzi wa maadili ya kitaifa ambapo kila mwananchi anapaswa kuishi kwa kuzingatia maono ya Baba wa Taifa yanayosisitiza uadilifu, haki, na uwajibikaji katika kila nyanja ya maisha.

Aidha, kudumisha umoja na utu ni msingi muhimu uliotujenga kama taifa linalojali heshima ya kila mtu bila ubaguzi, jambo ambalo ni muhimu katika kuepuka migogoro na kuimarisha utulivu wa ndani.

Vilevile, alizungumzia uzalendo katika maendeleo na amani ya nchi inategemea ushiriki wa dhati wa wananchi katika kujenga uchumi jumuishi, huku wakilinda rasilimali na miundombinu ya kimkakati ambayo ni mali ya taifa zima.

Mshikamano wa Watanzania ndio nguvu kuu, na kwa kumtazama Mwalimu Nyerere kama kielelezo cha uongozi unaojali utu na haki za binadamu kutasaidia kuvuka changamoto za sasa na kulifanya taifa kuendelea kuwa kimbilio la amani na utulivu barani Afrika na duniani kote.

No comments