RAIS DKT. SAMIA ASISITIZA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO AKIZINDUA MINARA 758 DODOMA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya mawasiliano nchini akiitaja kama rasilimali ya kimkakati kwa ajili ya uchumi na usalama wa taifa.

Katika hotuba yake, Rais amewataka wananchi na mamlaka husika kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa, huku akiagiza usimamizi wa huduma za mawasiliano uzingatie maadili, mila, na utamaduni wa Mtanzania.

Agizo hilo limetolewa leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano na maunganisho ya Mkongo wa Taifa katika wilaya 85 nchini, iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.

Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia ameshuhudia makabidhiano ya miundombinu hiyo kwa Serikali na kubainisha kuwa uwekezaji huo ni nguzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa kidigitali, hususan maeneo ya vijijini na mipakani.





Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa dunia inabadilika kwa kasi na mawasiliano si huduma ya anasa tena, bali ni msingi wa uchumi wa kisasa utakaofungua fursa za ajira na ubunifu kwa vijana. Ili kufanikisha hili, ameielekeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha wilaya zote ambazo bado hazijafikiwa na mkongo wa taifa zinaunganishwa kwa wakati, kabla ya juhudi kuelekezwa katika ngazi za chini zaidi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Aidha, Mheshimiwa Rais amezitaka halmashauri zote nchini kuondoa urasimu katika utoaji wa vibali vya miradi ya mawasiliano ili kuepuka kuongeza gharama za uwekezaji na kuchelewesha huduma kwa wananchi. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika ubunifu wa kidigitali ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Wakati huohuo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, ameeleza kuwa Mkongo wa Taifa umeshafika katika wilaya 121 kati ya 139 za Tanzania Bara, hatua inayoongeza uthabiti wa mawasiliano nchini.

No comments