WAZEE TAIFA WAIBARIKI RIPOTI YA TUME YA CHANDE, WAUNGA MKONO UCHUNGUZI WA JINAI

 


 

BARAZA la Ushauri la Wazee Taifa limepongeza ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, wakisema imeweka wazi ukweli na kutoa mwelekeo wa kudumisha amani nchini.

Akizungumza mjini Bariadi, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mzee David Sendo alisema tume hiyo imefanya kazi ya kina, yenye kuzingatia haki bila upendeleo, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuunda chombo hicho.

Alisema ripoti imegusa maeneo muhimu, ikiwemo kubaini kuwa baadhi ya kaulimbiu za kisiasa zilichangia kuchochea vurugu wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.

Sendo alisisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kujitathmini upya kuhusu lugha na kaulimbiu wanazotumia, akionya kuwa maneno yasiyo na tahadhari yanaweza kuleta taharuki badala ya kujenga mshikamano wa kitaifa.

Alivitaka vyama kuelekeza nguvu katika hoja zenye manufaa kwa wananchi na zinazolinda amani, hasa kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya teknolojia. Kuhusu pendekezo la kuundwa kwa tume ya kijinai kuchunguza wahusika wa vurugu hizo, alisema wazee wanaunga mkono hatua hiyo kwa asilimia 100 ili kuhakikisha waliohusika wanabainika na kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha, alipongeza juhudi za serikali kuwahudumia waathirika wa vurugu hizo, akisisitiza umuhimu wa kuwajumuisha pia wafanyabiashara wadogo waliopoteza mitaji yao ili waweze kurejea kwenye shughuli zao.

Wakati huo huo, wakazi wa Mwanza waliizungumzia ripoti hiyo na kuipongeza kwa kubaini ukweli, tofauti na taarifa zilizokuwa zikisambazwa awali na kusababisha taharuki katika jamii.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Machifu Tanzania, Mtemi Nyamironda III Aaron Mikomangwa alisema ripoti hiyo imeleta majibu sahihi kuhusu matukio ya vurugu, akiwataka wanasiasa kuepuka kauli zinazochochea hofu na badala yake kuheshimu matokeo ya tume.

Kwa upande wake, mkazi wa Mwanza, Mary Libaba alisema kuwekwa wazi kwa ukweli kumesaidia kutoa uelewa sahihi kwa wananchi, akionya kuwa wanaopinga ripoti hiyo wanaweza kuwa na nia isiyo njema.

No comments