TAKUKURU ,TASWA ZAUNGANA KUVALIA NJUGA RUSHWA KATIKA MICHEZO




Vitendo vya rushwa vimetajwa kuwa mmoja wa maadui wakubwa wanaorudisha nyuma maendeleo ya michezo nchini, huku maeneo ya usajili wa wachezaji, upangaji wa matokeo na uchezeshaji yakitajwa kuathiriwa zaidi na janga hilo. 

Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari za michezo iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) jana Aprili 24, Ofisa na Mkuu wa Uelimishaji Umma wa TAKUKURU mkoa wa Ilala, Mary Mwakyusa, amebainisha kuwa rushwa inaharibu misingi ya haki na ushindani wa kweli uwanjani.








Mwakyusa amesisitiza kuwa kumekuwa na matukio ya kusikitisha ambapo baadhi ya wadau hupokea hongo ili kupindisha taratibu na kutoa upendeleo kwa timu fulani, jambo linalofifisha vipaji na msisimko wa michezo. 

Amefafanua kuwa mapambano dhidi ya uovu huo si jukumu la Takukuru pekee, bali yanahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa wadau wote, hususan waandishi wa habari ambao wana wajibu wa kisheria na kimaadili kufichua maovu hayo kupitia kalamu zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taswa, Amir Mhando, amekiri kuwepo kwa pengo la habari za kiuchunguzi katika tasnia ya michezo, hali inayopelekea vitendo vingi visivyo halali kutokujulikana. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Taswa imewashirikisha wataalamu na magwiji wa habari nchini ili kuwajengea uwezo waandishi chipukizi na wakongwe namna ya kufanya uchunguzi wa kina, hatua inayotarajiwa kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika michezo kote nchini.

No comments