BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI YAHIMIZWA KASI UTOAJI HUDUMA SABASABA



Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Savera Salvatory, ameielekeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kuongeza kasi ya kutangaza huduma zake kwa wadau katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Sabasaba.

Bi. Savera amebainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuwahamasisha wanahabari wengi zaidi kujitokeza na kupata huduma za ithibati kwa urahisi, huku jamii ikipata uelewa mpana kuhusu majukumu ya bodi hiyo na umuhimu wa kuendesha shughuli za uandishi kwa kuzingatia misingi na taratibu za kitaaluma nchini.

Maelekezo hayo yametolewa wakati kiongozi huyo alipotembelea Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo maoneshoni hapo ili kujionea utendaji na huduma zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na kujionea  huduma na elimu inayotolewa kwa wananchi na wadau wanaotembelea maonesho hayo.

Katika banda la JAB Bi Savera alijionea huduma za ithibati, usajili pamoja na utoaji wa elimu kuhusu taaluma ya uandishi wa habari zinavyotolewa kwa waandishi na wananchi.

Katika ziara hiyo, Bi. Savera aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Bi. Zahra Guga, ambaye alimpongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, kwa usimamizi wake wa karibu wa shughuli za banda hilo kupitia ziara za mara kwa mara wakati wa maonesho.

Bi. Guga alisema uwepo wa viongozi katika banda la JAB unachochea uwajibikaji, huongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha utoaji wa elimu kwa wadau wanaotembelea maonesho ya Sabasaba.

No comments