WACHAMBUZI WAHIMIZA MASLAHI YA TAIFA MJADALA WA RIPOTI YA TUME YA CHANDE
WATANZANIA wametakiwa kujadili kwa kuweka mbele maslahi ya
taifa Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2025.
Akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa
na Kituo cha Utangazaji cha Uhai jijini Dar es Salaam, mchambuzi wa masuala ya
siasa nchini, Said Miraji alisema ripoti hiyo ni ajenda ya kitaifa na si mali
ya kundi au chama chochote cha siasa.
Alisisitiza kuwa masuala yaliyobainishwa, mapendekezo
yaliyotolewa na tume ikiwemo uwajibikaji, usawa na haki yanawahusu Watanzania
wote, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuyajadili kwa lengo la kujenga taifa
imara.
“Ni muhimu tukakaa na kuangalia mapendekezo yaliyotolewa
yana manufaa gani kwa wananchi, kwa pamoja tuyafanye kuwa ajenda ya kitaifa,”
alisema Miraji.
Aliongeza kuwa hata wale wasiokubaliana na uundwaji wa tume
hiyo wanapaswa kuzingatia yaliyomo kwenye ripoti kwa kuwa yanagusa maisha ya
wananchi moja kwa moja.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Dk
Faraja Kristomus alisema ripoti hiyo imeibua masuala mengi yaliyowakera hata
wananchi wasiokuwa na itikadi za vyama vya siasa wakati na baada ya uchaguzi
huo.
Alisisitiza kuwa mchakato wa kufikia muafaka wa kitaifa
haupaswi kuachwa mikononi mwa vyama vya siasa pekee, bali unahitaji ushiriki
mpana wa wananchi wote.
Aidha, Dk Kristomus alibainisha kuwa katika safari ya
kufikia maridhiano ya kitaifa, ni muhimu wananchi kushiriki kikamilifu katika
majadiliano ili kuhakikisha ajenda zinazojadiliwa zinanufaisha taifa zima,
badala ya makundi maalumu.
Alionya dhidi ya hali ambapo kundi fulani linaweza kujiona
lina mamlaka ya kumiliki mifumo ya utawala, akisisitiza umuhimu wa kuendelea
kutoa elimu ya uraia na uzalendo ili wananchi watambue haki zao na
kuwawajibisha viongozi. Akizungumzia matukio ya uchaguzi huo, alisema yalikuwa
ni matokeo ya matatizo yaliyokuwa yakipuuzwa kwa muda mrefu. “Yaliyotokea
Oktoba 29 yalikuwa kama bomu lililopasuka baada ya kukaa muda mrefu bila
kuteguliwa,” alisema Dk Kristomus.
Aliwahimiza Watanzania kujifunza kutokana na yaliyotokea na
kuchukua hatua za kutekeleza makubaliano yatakayofikiwa ili kuepusha migogoro
isiyo na tija siku zijazo.

Post a Comment