WATANZANIA WATAKIWA KUTOKUBALI KURUDISHWA NYUMA KUSAKA AMANI NA UTULIVU
Siku moja
baada ya kutolewa kwa ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea wakati
na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, hali ya usalama nchini imeendelea kuwa
shwari huku wananchi wakitekeleza majukumu yao ya kila siku kama kawaida.
Mamilioni ya Watanzania
waliofuatilia uwasilishwaji wa ripoti hiyo na mapendekezo yake wameonesha kuwa
na matumaini makubwa ya kusonga mbele, wakigubikwa na hisia za kuumizwa na
ghasia zilizojitokeza kipindi hicho lakini wakiwa na dhamira ya kutorejea huko
tena.
Hata hivyo,
vyama vikuu vya upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
pamoja na ACT Wazalendo, vimejitokeza hadharani kuipinga kazi iliyofanywa na
Tume hiyo kupitia matamko yao kwa umma.
Pamoja na malalamiko hayo,
uchambuzi wa kina unaonesha kuwa hoja zinazotolewa na vyama hivyo ni dhaifu
ikilinganishwa na mustakabali wa Taifa na ukweli wa madhara yaliyopatikana,
hasa ikizingatiwa kuwa hali ya nchi ilikuwa shwari kabla ya kupandikizwa kwa
mbegu za chuki na chokochoko za ghasia zilizoratibiwa takribani miezi sita
kabla ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa
taarifa hiyo ya uchunguzi, ghasia hizo zilipangwa na kufadhiliwa na watu
waliopata mafunzo maalumu, jambo ambalo limewafanya Watanzania walio wengi
kutamani kurejea kwenye amani yao ya asili na kukataa kutumika kama nyenzo ya
wanasiasa kwa maslahi binafsi.
CHADEMA inadai kuwa Tume hiyo si
chombo huru kwa madai kuwa imeundwa chini ya Sheria ya Uchunguzi ya mwaka 2002
inayompa Rais mamlaka ya kuiongoza, lakini ufafanuzi wa kisheria unaonesha kuwa
Tume ina kinga na uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa, ikiwa na mamlaka sawa
na Mahakama Kuu katika kukusanya ushahidi.
Upande wa ACT
Wazalendo nao umetoa hoja zinazofanana na hizo ukidai Tume iliundwa kulinda
wahusika, hoja ambayo inakosa mashiko kwani ripoti imegusia masuala ya
uwajibikaji kwa uwazi.
Vyama hivi vinaonekana kuyumba
baada ya mikakati yao kutofua dafu, huku uamuzi wao wa kususia mchakato wa Tume
ukiwanyima fursa ya kusikilizwa .Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mohamed Chande
Othman, alieleza kuwa zaidi ya watu 63,000 walifika kutoa ushahidi ilikuwa ni
fursa kwa kila mwananchi kushiriki.
Kwa sasa, huku
wawakilishi wa taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola
wakiahidi kushirikiana na Tanzania katika hatua hii, ni dhahiri kuwa hoja za
kupuuza mchakato wa ndani hazina msingi imara.
Ni muhimu kwa Watanzania kuendelea
kuwa macho na kuwakataa wanasiasa wanaojaribu kuwatumia kwa maslahi yao, ili
kuhakikisha kuwa changamoto na machungu yaliyopita hayajirudii tena katika
historia ya nchi yetu.
Post a Comment