MAANDALIZI AFCON 2027 YAFIKIA HATUA NZURI MIUNDOMBINU IKIIMARIKA
Serikali imetoa ripoti ya matumaini kuhusu maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ikibainisha kuwa ujenzi na ukarabati wa viwanja muhimu nchini umepiga hatua kubwa.
Katika maendeleo hayo, Uwanja wa Arusha umefikia asilimia 78 ya ujenzi wake huku uwanja wa Fumba ukiwa umefika asilimia 60, wakati ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiendelea kwa ajili ya kubadilisha sehemu ya kuchezea ili kukidhi vigezo vya kimataifa.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, mara baada ya kukamilisha kikao cha kimkakati mjini Kampala, Uganda, kilichomkutanisha na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Samson Adamu.
Kikao hicho kilihusisha nchi zote tatu wenyeji wa mashindano hayo ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda, lengo likiwa ni kutathmini utayari wa miundombinu ikiwemo barabara na hoteli ambazo zimeshaandaliwa kwa ajili ya kupokea wageni.
Naibu Waziri Mwinjuma amesisitiza kuwa suala la kuhamishwa kwa mashindano hayo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki halipo, badala yake nchi wanachama zimekubaliana kuunda Kamati ya Maandalizi ya Pamoja itakayofanya kazi na kamati za ndani za kila nchi.
Hatua hiyo inalenga kufanya mashindano ya AFCON 2027 kuwa ya kihistoria, yakihusisha umoja thabiti na uwajibikaji wa pamoja miongoni mwa mataifa haya matatu kwa mara ya kwanza.
Aidha, mijadala katika kikao hicho ilijikita pia katika kuchukua uzoefu kutoka kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) iliyomalizika hivi karibuni ili kuboresha utendaji. Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa kila kitu kiko sawa na imejipanga kuhakikisha jamii inashirikishwa kikamilifu ili mashindano haya yaweze kuleta tija ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa zima.
Post a Comment