WASTAAFU KIKWETE, CHAKWERA WATETA DAR

 



 Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amefanya mazungumzo mazito na Rais Mstaafu wa Malawi na Mjumbe Maalum wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), Dkt. Lazarus Chakwera, yenye lengo la kuimarisha misingi ya hali ya kisiasa nchini.

Katika mkutano huo uliofanyika ofisini kwa Dkt. Kikwete jijini Dar es Salaam mnamo Aprili 15, 2026, viongozi hao wawili wamejadili mustakabali wa amani na utulivu wa Tanzania, huku wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo jumuishi katika kutatua changamoto za kisiasa zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Dkt. Chakwera yupo nchini tangu Aprili 8 chini ya utaratibu wa "Good Offices" wa Commonwealth, akitekeleza jukumu lake la kusaidia juhudi za kidiplomasia kupunguza mivutano na kujenga maridhiano ya kitaifa.

Ziara hii ya Dkt. Chakwera imekuwa na tija kubwa kwani mbali na kukutana na Dkt. Kikwete, tayari ameshafanya mazungumzo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau mbalimbali wa siasa, asasi za kiraia, na viongozi wa dini nchini.

Jukumu alilopewa na Katibu Mkuu wa Commonwealth, Bi. Shirley Ayorkor Botchwey, ni kusaidia kuweka msingi wa majadiliano jumuishi yatakayochochea maboresho ya mifumo ya utawala na kudumisha utulivu wa muda mrefu.

Hatua ya kukutana na Dkt. Kikwete, ambaye ana uzoefu mpana wa kidiplomasia na maridhiano barani Afrika, inaashiria dhamira ya dhati ya kurejesha umoja wa kitaifa na kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele kwa amani na mshikamano.

 

No comments