WANAHABARI WATAKIWA KUTUMIA ‘KALAMU’ ZAO KUJENGA TAIFA, KUKUZA AMANI




Waandishi wa habari nchini wamehimizwa kutumia majukwaa yao kama nyenzo madhubuti ya kujenga taifa na kuimarisha mshikamano, badala ya kusambaza maudhui yanayoweza kuigawa jamii. 

Rai hiyo imetolewa na Dkt. Egbert Mkoko kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati akiwasilisha mada kuhusu uandishi wa habari unaojenga nchi katika kikao cha wadau wa sekta hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana Aprili 17.

Dkt. Mkoko amesema kuwa uandishi wa habari ni nguvu kubwa inayoweza kuunganisha watu na kuchochea maendeleo, lakini inaweza pia kusababisha machafuko iwapo itatumiwa bila umakini na weledi. Amesimamia hoja kuwa taifa lolote hujengwa na simulizi zake, hivyo ni wajibu wa wanahabari kusimulia hadithi zinazounganisha na kuelimisha umma.

Akifafanua wajibu wa waandishi, Dkt. Mkoko amesisitiza umuhimu wa kuhakiki ukweli wa taarifa kabla ya kuzichapisha na kuzingatia maadili ya taaluma. Amewataka wanahabari kuelekeza nguvu zaidi katika kuibua suluhisho la changamoto za kijamii na kuonyesha mafanikio ya maendeleo, badala ya kuangazia matatizo pekee.

Aidha, ametoa onyo kali dhidi ya matumizi ya lugha za chuki, habari za uongo, na uandishi wa kusisimua kupita kiasi (sensationalism). Amesema kuwa upotoshaji wa namna hiyo si tu unaharibu taswira ya vyombo vya habari, bali pia unahatarisha utulivu wa nchi na kupoteza imani ya wananchi kwa vyombo hivyo.

Katika kuelekea kwenye uandishi wa habari za maendeleo, mtaalamu huyo amevitaka vyombo vya habari kuweka mikakati madhubuti ikiwemo mifumo ya uhakiki wa taarifa (fact-checking) na mafunzo endelevu kwa wafanyakazi wao. Amewaasa wahariri kusimama imara kama walinzi wa maudhui ili kuhakikisha kila habari inayotoka inazingatia maslahi mapana ya taifa na utulivu wake.

No comments