RAIS AFRIKA KUSINI HAKUNA KULALA BAFANA BAFANA

 


Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amewatumia ujumbe wa hamasa wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu Bafana Bafana, kuelekea mechi ya hatua ya 32 Bora katika Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Canada itakayopigwa leo Jumapili, Juni 28, 2026.

Katika ujumbe huo, Rais Ramaphosa amewataka wachezaji kuingia uwanjani kwa kujiamini na kupambana kishujaa ili kuipeperusha vyema bendera ya Afrika kusini. Amewasihi Waafrika Kusini wote kujitokeza kwa wingi na kuungana kwa pamoja kuishabikia timu yao katika hatua hii muhimu ya mtoano.

Kiongozi huyo hakusita kutia maneno ya utani ya kiungwana wa kidiplomasia kwa kumtumia ujumbe wa tahadhari Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, akimueleza kuwa, ingawa nchi zao zina urafiki mkubwa wa kidiplomasia, urafiki huo utawekwa kando kwa dakika 90 uwanjani huku akitamba kuwa Bafana Bafana iko tayari kuzima cheche za miamba hiyo ya Amerika Kaskazini. Ujumbe huo umepokelewa kwa hisia chanya na mashabiki wengi mitandaoni huku ukiongeza presha na msisimko mkubwa kuelekea mchezo huo wa kukata na shoka.

Mechi hiyo itakayopigwa saa 4:00 usiku kwenye uwanja wa Los Angeles, inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute huku kila timu ikisaka tiketi ya kusonga mbele kwenye hatua ya 16 bora ya michuano hiyo mikubwa duniani.

No comments