ZAIDI YA WANAFUNZI 3,000 WA SHULE YA MSINGI CHARAMBE KUNUFAIKA NA JIKO LA KISASA LA NISHATI SAFI
Zaidi ya wanafunzi 3,000 wa Shule ya Msingi Charambe iliyopo jijini Dar es Salaam wanatarajia kunufaika kwa kupata chakula safi na salama kwa wakati, kufuatia uzinduzi wa jiko jipya la kisasa linalotumia nishati safi ya gesi, mradi uliotekelezwa na Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam Sunset kwa kushirikiana na kampuni ya PWC kupitia Mradi wa Jiko Safi (Clean Energy Project).
Mradi huo umeleta mapinduzi makubwa shuleni hapo kwa kuondoa kabisa mfumo wa zamani wa kupikia kwa kutumia kuni uliokuwa ukihatarisha afya zao na kubadilishwa kuwa wa nishati ya gesi ambayo inapunguza athari za moshi kwa watoto na wapishi, huku ikitunza mazingira kwa kuzuia ukataji miti.
Mbali na jiko hilo litakalohakikisha maelfu ya wanafunzi hao wanapata lishe katika mazingira salama, klabu hiyo ilitoa msaada wa sufuria kubwa, mitungi ya gesi, vifaa vya kupikia, na kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya vyoo vya wanafunzi kwa kuweka milango mipya, kurekebisha sakafu, na kupaka rangi.
Vilevile, ili kuboresha zaidi mazingira ya kujifunzia ya wanafunzi hao, wadau hao walikabidhi madawati mapya 100 na kukarabati mengine 78 yaliyokuwa yameharibika, hatua iliyosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa changamoto ya watoto kukaa chini darasani, huku wakigawa jezi za michezo na kupanda miti shuleni hapo kwa kushirikiana na Rotary E-Club of East Africa.
Akizungumza kwa niaba ya shule hiyo, Bi. Elizabeth Mganga alieleza kuwa msaada huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa shule hiyo iliyoanzishwa Julai 2004 ikiwa na wanafunzi 2,030, na ambayo sasa inahudumia watoto 3,233 ikiwa na walimu 48, kwani idadi ya madawati sasa imeongezeka hadi kufikia 636 na kufanya mazingira ya masomo kuwa ya kuvutia.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Bw. Jomari Satura, aliipongeza klabu hiyo na PWC kwa kugusa maisha ya maelfu ya watoto wa Charambe, huku Rais wa Rotary Club of Dar es Salaam Sunset, Tahir Othman, akihitimisha kwa kusisitiza kuwa mradi huo ni uwekezaji wa kudumu katika afya na ustawi wa watoto ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao kupitia elimu bora.

Post a Comment