SAMIA AFUNGUA MILANGO YA UTAJIRI BAHARINI: MELI NYINGINE NNE ZAJA

 


Na Mwandishi Wetu, BSKYmedia

Serikali imetangaza neema kubwa kwa wadau wa uchumi wa buluu nchini baada ya kubainisha kuwa mbali na meli ya kisasa iliyozinduliwa, mchakato wa kununua meli nyingine nne za uvuvi wa bahari kuu upo mbioni kukamilika ili kuongeza nguvu ya uvunaji wa rasilimali za majini. 

Katika mkakati huo mzito wa kuneemesha uchumi wa nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa serikali imejipanga kukamilisha ujenzi wa bandari mbili kubwa na za kimkakati za uvuvi katika maeneo ya Kilwa na Bagamoyo. Hatua hiyo inalenga kuimarisha ushindani wa sekta ya uvuvi nchini na kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na miundombinu ya kisasa itakayowezesha meli kubwa kutia nanga na kuchakata mazao ya baharini hapa nchini badala ya kuishia nje ya nchi.

Uzinduzi huo wa Mpango na Mfumo wa Kuimarisha Uvuvi wa Bahari Kuu umeambatana na kukabidhi meli mpya yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 7, ambayo ni matunda ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Japan. 

Meli hiyo itaiwezesha nchi kuvua samaki waliopo kwenye  ukanda maalum wa uchumi wa bahari (EEZ) ambao awali haukuweza kufikiwa kutokana na kukosekana kwa meli ya aina hiyo.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika Aprili 25,2026 kwenye ufukwe wa Makao makuu ya Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) Kigamboni mkoani Dar-es-salaam , Mhe. Rais Samia pia amesema kuwa hatua hiyo inalenga kukuza fursa za ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha lishe.






Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali imedhamiria kuleta mageuzi ya kiteknolojia, ikiwemo uenezaji wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Bahari ya Hindi ili kutoa ajira na kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja. 

Akizungumza kwa kusisitiza, Rais amewataka Watanzania "kukaa mguu sawa" kwani huu ni mwanzo wa safari ndefu ya kuitawala bahari kuu, huku akionya kuwa ulinzi utaimarishwa kudhibiti uvuvi haramu ili rasilimali hizo ziwanufaishe wananchi wa sasa na na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, uongozi wa wizara na wadau wa maendeleo wameelezea utayari wao wa kusimamia mifumo hiyo mipya ili kuleta tija inayokusudiwa kupitia uchakataji, mafunzo, na utafiti wa kisasa. 

Kwa upande wake, Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Bashiru Ally Kakurwa, ameeleza kuwa wizara imejipanga kikamilifu kuunga mkono maono ya Rais kwa kuimarisha mifumo ya uzalishaji na kutoa mafunzo ya kisasa kwa wavuvi ili kuongeza thamani ya mazao ya baharini. 

Mafanikio haya pia yameungwa mkono na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao wamechangia katika kuimarisha mnyororo wa thamani.

No comments