TANZANITE JUNIOR CHESS CHAMPIONSHIP YALETA MAPINDUZI YA MCHEZO DAR

 


Mchezo wa Chess umetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kukuza uwezo wa watoto kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi, sifa ambazo ni msingi wa mafanikio darasani na katika maisha ya kila siku. Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Klabu ya Chess ya Tanzanite Legacy, Hellen Ulaya, wakati wa mashindano ya Tanzanite Junior Chess Championship yaliyofanyika jijini hapa yakishirikisha wachezaji kutoka shule mbalimbali nchini.

Hellen ameeleza kuwa ushiriki wa wazazi ni nguzo muhimu katika kukuza vipaji vya watoto, huku akisisitiza kuwa mchezo huo unajenga nidhamu na umakini mkubwa. Alifafanua kuwa lengo kuu la mashindano hayo ni kuibua na kukuza vipaji vya chess tangu wakiwa wadogo, ili kuandaa kizazi chenye fikra makini kitakachoweza kuiwakilisha Tanzania vyema katika anga za kimataifa.





 

Mbali na kukuza akili, mashindano hayo yanalenga kuhamasisha ujifunzaji kupitia michezo, huku yakijenga urafiki, ushirikiano, na ushindani wenye afya miongoni mwa washiriki. Hellen aliongeza kuwa kila mtoto anastahili kupata fursa ya kushiriki michezo ya maendeleo ya akili bila kujali hali ya kifedha, na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana na klabu hiyo ili kueneza mchezo wa chess mashuleni na katika jamii kwa upana zaidi.

Mashindano ya Tanzanite Junior Chess Championship sasa yanatarajiwa kufanyika kila mwaka, yakilenga kuendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa watoto na kutoa jukwaa la kudumu kwa vipaji vipya kuonekana na kuendelezwa nchini.

No comments