MUSEVENI: UGANDA IKO TAYARI KULINDA AMANI NA MARIDHIANO SUDAN KUSINI

 



 Serikali ya Uganda imetangaza kuwa iko tayari kuhakikisha amani na maridhiano ya kudumu yanapatikana nchini Sudan Kusini, ili kulinda usalama wa raia na kukuza ustawi wa kiuchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.

Msimamo huo umetolewa na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, alipofanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, katika Ikulu ndogo ya Nakasero jijini Kampala. Dkt. Kikwete amemtembelea Rais Museveni akiwa katika jukumu lake jipya kama Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.





Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamesisitiza kuwa suluhu ya kudumu ya mzozo wa Sudan Kusini inategemea utayari wa pande zinazovutana kuketi kwenye meza ya mazungumzo. Rais Museveni amebainisha kuwa utulivu wa nchi hiyo, hususan katika jimbo la Equatoria lenye idadi kubwa ya raia wa Uganda, ni kiungo muhimu cha usalama wa mipakani na biashara za kikanda.

Kwa upande wake, Dkt. Kikwete amewasilisha mikakati ya Umoja wa Afrika inayolenga kuleta upatanishi na utatuzi wa migogoro katika eneo hilo lenye changamoto nyingi za kisiasa. Juhudi hizi zinakuja wakati muafaka ambapo AU inatafuta suluhu za ndani ya bara la Afrika kwa matatizo ya Waafrika.

Kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kidiplomasia na rekodi ya muda mrefu katika kusimamia amani barani Afrika, uteuzi wa Dkt. Kikwete katika nafasi hiyo unatajwa kuwa chachu itakayoimarisha ushirikiano wa kikanda na kuleta msukumo mpya wa amani katika Bahari ya Shamu na maeneo jirani.

No comments