TANZANIA YAADHIMISHA MIAKA 62 YA MUUNGANO KWA KUELEKEZA FEDHA ZA SHEREHE KWENYE MIUNDOMBINU




Tanzania leo imeadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa utulivu nchi nzima, huku kipaumbele kikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukarabati wa miundombinu. 

Rais Samia Suluhu Hassan ameahirisha shamrashamra za sherehe kitaifa na kuelekeza fedha zilizokuwa zimetengwa zitumike kurekebisha barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, hatua ambayo imetajwa na wananchi kama uamuzi wa busara unaolenga kutatua kero za dharura za kijamii.

Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akizungumza mkoani Unguja Kusini, amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu kulinda amani na usalama wa taifa kama msingi mkuu wa kudumisha Muungano huo ulioasisiwa Aprili 26, 1964. 

Katika maadhimisho hayo, Serikali imezindua jengo jipya la Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati na kuweka jiwe la msingi la miradi ya elimu ya juu Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha huduma na mshikamano wa kitaifa upande wa visiwa na bara.

Hatua ya maridhiano na utatuzi wa kero za Muungano imepiga hatua nyingine leo kufuatia kuondolewa kwa kero ya uingizaji sukari kutoka Zanzibar kwenda soko la Tanzania Bara baada ya kutiwa saini kwa hati ya makubaliano mjini Unguja. 

Wadau na wachambuzi wa siasa wamepongeza hatua hiyo wakisema kuwa kupungua kwa hoja za Muungano hadi kubaki tatu pekee ni ushahidi wa kukomaa kwa uongozi na dhamira ya dhati ya kuimarisha undugu wa kihistoria kati ya pande hizo mbili.

Wananchi na wastaafu waliohojiwa wamesisitiza kuwa Muungano wa sasa umevuka mipaka ya kisiasa na kuwa muungano wa mioyo kupitia mwingiliano wa kifamilia na biashara, huku wakitoa wito wa kudhibiti chokochoko zinazolenga kubomoa amani ya nchi. 

Aidha, wametoa ushauri kwa serikali kuimarisha somo la uzalendo katika mitaala ya elimu ili kuwajengea vijana msingi imara wa kuuenzi Muungano kama urithi adhimu uliopatikana kwa gharama kubwa ya busara za waasisi, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, wakishuhudia utiaji Saini wa kuondoa hoja ya Uingizaji wa Sukari kutoka Zanzibar katika Soko la Tanzania Bara katika orodha ya hoja za Muungano. Makubaliano hayo yamefanyika wakati wa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia Masuala ya Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar,  Aprili 25 , 2026.

No comments