RAIS SAMIA ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 1,369 KUADHIMISHA MIAKA 62 YA MUUNGANO



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametumia mamlaka yake kikatiba kutoa msamaha kwa jumla ya wafungwa 1,369 nchi nzima katika kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili, 2026. 

Msamaha huo uliotolewa chini ya Ibara ya 45 ya Katiba ya nchi, unahusisha wafungwa walioachiwa huru moja kwa moja pamoja na wale waliopunguziwa sehemu ya adhabu zao za vifungo gerezani. 

Katika msamaha huo, wafungwa 436 wameachiwa huru kuanzia leo, huku wafungwa wengine 933 wakipunguziwa adhabu zao kwa asilimia 16 (moja ya sita) ya vifungo vyao na kubaki gerezani kuendelea kutumikia sehemu iliyobaki ya adhabu hiyo.

Wafungwa walionufaika na hatua hiyo ya Rais ni pamoja na wale waliokuwa wakitumikia vifungo vya mwaka mmoja na kuendelea ambao tayari wameshatumikia robo ya adhabu zao na walikuwa gerezani kabla ya tarehe 25 Januari, 2026. 

Aidha, msamaha huo umewagusa wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu walio katika hatua ya mwisho ya ugonjwa, wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, pamoja na wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa na ujauzito au wenye watoto wanaonyonya. Makundi mengine ni wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi, wafungwa waliokuwa chini ya uangalizi wa Rais kwa miaka kumi au zaidi, na wale waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa kwa miaka 15 na kuendelea ambao sasa adhabu zao zimebadilishwa kuwa kifungo cha maisha.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Paschal Katambi, amebainisha kuwa msamaha huo haujawagusa wafungwa waliohukumiwa kwa makosa mazito yakiwemo uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji fedha, na rushwa. 

Vilevile, wafungwa wa makosa ya usafirishaji wa binadamu, biashara ya dawa za kulevya, kubaka, kulawiti, wizi wa watoto, unyang’anyi wa kutumia nguvu au silaha, pamoja na makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu hawakunufaika na msamaha huu. Makosa mengine yaliyozuiwa ni pamoja na ujangili, wizi wa fedha za serikali, makosa ya kigaidi, uharamia, makosa ya kimtandao, na wale waliohukumiwa kwa makosa ya kujaribu kuua au kujiua.

Serikali imesisitiza kuwa wafungwa waliowahi kupata msamaha wa Rais huko nyuma, wafungwa wa madeni, na wale waliopata makosa ya kinidhamu gerezani ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita pia wameachwa nje ya msamaha wa sasa. 

Waziri Katambi ametoa rai kwa wafungwa wote walioachiwa huru kurejea katika jamii na kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa, huku akiwasihi kuepuka vitendo vya kihalifu ili wasirejee tena gerezani. Hatua hiyo ya Rais Samia imeelezwa kuwa ni sehemu ya dhamira ya serikali katika kuimarisha utu, umoja na msamaha wa kitaifa kuelekea muongo mwingine wa mafanikio ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


No comments