SIMBA YAREJEA NAFASI YA PILI, YAIWEKEA YANGA SHINIKIZO LA POINTI NNE

 



KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameeleza kufurahishwa na kiwango cha timu yake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union, mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es Salaam. 

Ushindi huo umeifanya Simba kurejea rasmi katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikifikisha pointi 34 baada ya michezo 15.

Matokeo hayo yameongeza shinikizo kwa mahasimu wao, Yanga, wanaoongoza ligi kwa pointi 38 katika michezo 16, huku Simba ikiwa na faida ya mchezo mmoja mkononi. 

Akizungumza mara baada ya filimbi ya mwisho, Barker alisema kuwa kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya wapinzani wao ni sehemu ya mkakati wao wa kurejesha heshima ya ubingwa msimu huu.

"Lengo letu ni kushinda ubingwa msimu huu, na hatuwezi kufanikisha hilo kama hatutashinda mechi zetu. Nimefurahishwa na matokeo haya na nawapongeza wachezaji wangu kwa kupambana," alisema Barker.

 Hata hivyo, kocha huyo alibainisha kuwa bado kuna mapungufu ya kiufundi, akitaja upotevu wa mipira mara kwa mara kama changamoto anayoenda kuifanyia kazi haraka katika uwanja wa mazoezi.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mohamed Muya, alikubali matokeo hayo huku akilaumu ukosefu wa umakini katika safu yake ya ushambulizi. 

Muya alisema kuwa wachezaji wake walishindwa kufanya maamuzi sahihi kwenye "mipira ya mwisho" (final third), jambo lililowagharimu na kuwafanya washindwe kupata hata bao la kufutia machozi mbele ya wekundu wa Msimbazi.

No comments