WANAANGA WA ARTEMIS 2 WASOGEA KARIBU ZAIDI NA MWEZI KULIKO DUNIA
Wanaanga wanne wa misheni ya NASA ya Artemis 2 wamefikia hatua muhimu katika safari yao baada ya kutangazwa kuwa sasa wapo karibu zaidi na Mwezi kuliko walivyo na sayari ya Dunia.
Taarifa hiyo ya kusisimua ilitolewa usiku wa manane kuamkia leo Jumamosi, Aprili 4, na Jacki Mahaffey, kutoka Kituo cha Anga za Juu cha Johnson mjini Houston.
Akipokea habari hizo kwa furaha, mtaalamu wa misheni hiyo, Christina Koch, alieleza kuwa kikundi hicho kilijawa na nderemo huku wakitazama uzuri wa Mwezi kupitia dirisha la chombo chao cha Orion, wakivutiwa na mandhari ya upande wa mbali wa Mwezi ambayo yanaendelea kuonekana wazi zaidi.
Safari hiyo iliyoanza Jumatano, Aprili 1, inawajumuisha wanaanga wa NASA Christina Koch, Reid Wiseman, Victor Glover, na mwanaanga wa Shirika la Anga la Canada, Jeremy Hansen.
Inatarajiwa kuwa ifikapo Jumatatu, Aprili 6, mashujaa hawa watazunguka upande wa mbali wa Mwezi, umbali ambao utaweka rekodi mpya ya binadamu kusafiri mbali zaidi na Dunia kuliko ilivyowahi kutokea huko nyuma.
Kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani Aprili 10, wanaanga hao watakuwa wametumia muda wao kuandaa vifaa vya kisayansi, kufanya mazoezi ya viungo, na kufurahia mandhari ya kipekee ya anga za juu ambayo wachache hupata fursa ya kuiona.

Post a Comment