MOTSEPE AJIVUNIA AFRIKA KUPELEKA TIMU 10 KOMBE LA DUNIA MAREKANI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, ameeleza fahari yake kutokana na bara la Afrika kutoa idadi ya kihistoria ya wawakilishi 10 katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka huu nchini Marekani, Canada, na Mexico.
Akizungumza jijini Cairo, Misri, Motsepe amebainisha kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho tosha wa kukua kwa kasi kwa kiwango cha soka barani Afrika na ushindani wa kimataifa.
Katika fainali hizo zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia mwezi Juni hadi Julai, mataifa 10 yatakayopeperusha bendera ya Afrika ni Ghana, Cape Verde, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ivory Coast, Afrika Kusini, Misri, Morocco, Tunisia, na Algeria.
Motsepe amesisitiza kuwa CAF inajivunia hatua hiyo kubwa na ina imani thabiti kuwa timu hizo zitafanya vizuri na kuleta ushindani wa kweli dhidi ya mataifa mengine makubwa duniani.
Moja ya vivutio vikubwa katika orodha hiyo ni timu ya taifa ya DRC, ambayo Rais Motsepe ameipongeza kwa namna ya kipekee baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Jamaica na kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974. Mafanikio ya DRC yameonekana kama ishara ya mabadiliko chanya ya soka katika ukanda wa Afrika ya Kati, huku yakirejesha matumaini ya nchi hiyo katika ramani ya soka la dunia baada ya kusubiri kwa zaidi ya miongo mitano.
Rais huyo wa CAF amehitimisha kwa kusema kuwa kuongezeka kwa idadi ya timu kutoka Afrika ni matokeo ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na usimamizi bora wa soka ndani ya shirikisho hilo. Amesema kuwa macho ya ulimwengu sasa yameelekezwa kwa wawakilishi hao kumi, akiamini kuwa Afrika inaweza kuweka rekodi mpya ya kufika hatua za juu zaidi katika mashindano hayo makubwa duniani.

Post a Comment