SERENGETI GIRLS YATANGULIZA MIGUU MIWILI KOMBE LA DUNIA, YAIPIGA BOTSWANA KWAO



TIMU ya taifa ya wasichana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, ‘Serengeti Girls’, imeanza kampeni ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa kishindo baada ya kuichapa Botswana mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume mjini hapa.

Katika mchezo huo uliopigwa ugenini, Serengeti Girls walionyesha dhamira ya ushindi mapema ambapo walifanikiwa kupata mabao yote matatu ndani ya kipindi cha kwanza. Fatuma Hassan alikuwa wa kwanza kucheka na nyavu dakika ya 15, akifuatiwa na Bahati Steven dakika ya 40, huku Zuhura Mlekwa akihitimisha karamu hiyo ya mabao dakika ya 45.

Wenyeji Botswana walipata bao lao la kwanza dakika ya 42, na kurejea kwa kasi kipindi cha pili ambapo waliongeza bao la pili kwa mkwaju wa penalti. Hatua hiyo ilifanya mchezo kuwa wa ushindani mkali huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, lakini mabinti wa Kitanzania walisimama imara na kulinda ushindi huo muhimu ugenini.

Timu hizi zinatarajiwa kurudiana jijini Dar es Salaam ifikapo Aprili 19, mwaka huu. Mshindi wa jumla wa mpambano huo atafuzu hatua inayofuata kukabiliana na Afrika Kusini, ambapo mshindi kati yao atacheza na mshindi wa mechi kati ya Kenya na Uganda ili kupata tiketi ya kwenda Morocco.

Serengeti Girls wanapambana kurejea kwenye ramani ya dunia kwa mara ya pili, baada ya kuandika historia ya kushiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza mwaka 2022 nchini India.

No comments