SASA RASMI AFCON 2027 NI JUNI 19



SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limethibitisha rasmi kuwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) zitatarajiwa kuanza Juni 19 na kufikia kilele Julai 18 mwaka ujao, huku zikiandika historia mpya kwa kuandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika kuandaliwa kwa pamoja na mataifa matatu, hatua inayotajwa kuwa na tija katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda pamoja na kuongeza ushindani wa hali ya juu.

Michuano hiyo inatarajiwa kuwa ya kipekee kutokana na mabadiliko ya kimfumo, ambapo idadi ya timu zinazoshiriki itaongezeka kufikia timu 28, tofauti na timu 24 zilizoshiriki katika msimu uliopita nchini Morocco. Aidha, AFCON ya mwaka 2027 itakuwa ya mwisho kufanyika kwa mfumo wa kila baada ya miaka miwili, kwani kuanzia mwaka 2028 michuano hiyo itahamia rasmi kwenye utaratibu wa kufanyika kila baada ya miaka minne.

Tukio hili pia linaashiria kurejea kwa michuano hiyo katika ukanda wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya kupita takribani miongo mitano tangu ilipofanyika mara ya mwisho mwaka 1976 nchini Ethiopia.

Tayari maandalizi ya awali yameshaanza kushika kasi katika nchi zote tatu husika, ambapo serikali kwa kushirikiana na mashirikisho ya soka zinaendelea kuboresha miundombinu na viwanja ili kuhakikisha vinakidhi viwango vya kimataifa vinavyotakiwa na CAF kabla ya kuanza kwa kishindo kwa mashindano hayo.

No comments